We ought to do good to others as simply as a horse runs, or a bee makes honey, or a vine bears grapes season after season without thinking of the grapes it has borne. – Marcus Aurelius

Ni siku nyingine nzuri, siku ya mafanikio, siku ambayo tumepata nafasi nzuri na ya kipekee ya kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Msingi wetu wa maisha ya mafanikio ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA ambapo tunakwenda kufanya nakubwa leo na kila siku ya maisha yetu.

Asubuhi ya leo tutafakari SABABU YA KUWA MWEMA KWA WENGINE…
Swali, ni sababu gani inayoweza kukupelekea wewe kuwafanyia watu wema?
Ni kipi hasa kitakachokusukuma wewe uwatendee wengine wema?
Unaweza kuwa na majibu yako, lakini jibu sahihi ni moja; HAKUNA SABABU.
Unapaswa kuwa mwema kwa wengine bila sababu yoyote.
Huhitaji sababu kuwa mwema, unahitaji kuwa mwema, kwa sababu hilo ndiyo jukumu lako.

Unakula asali na kuifurahia ni tamu, je unafikiri nyuki walitengeneza asali hiyo tamu kwa sababu yako?
Unapokula embe na kufurahia utamu wake, unaelewa kabisa mwembe uliotoa embe unalokula haujui hata kama wewe ndiye unayekula embe hilo.

Kila kiumbe hai kwa asili yake, kinafanya kile ambacho kinapaswa kufanya.
Kadhalika na sisi binadamu, tunachopaswa kufanya ni kuwa wema kwa wengine. Hivyo tunapaswa kuwa wema, bilanya sababu yoyote. Tuwe wema kwa kila mtu, kwa sababu ndiyo ubinadamu huo.

Ukawe mwema leo kwa kila unayekutana naye, bila ya sababu yoyote.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kurasa