Hata kitu kizuri, kikifanyika kupita kiasi, kinakuwa madhara. Kila kitu kinapaswa kufanywa kwa kiasi, na kiasi sahihi cha kufanya ni changamoto kwa wengi.

Hata utafutaji wa fedha, unapaswa kufanya kwa kiasi, ili uweze kuendelea na zoezi hilo na muhimu zaidi, usiwe mtu wa kupata wewe tu na wengine wakakosa.

Watu wengi wanaopotelea kwenye mambo ambayo tunaona wamepotea, wengi hawakuwa na lengo la kupotea. Walianza kidogo kwa nia njema, lakini tatizo kubwa ni kwamba hawakujua ni wakati gani wa kuacha.

wp-image--1475273682

Kama ilivyo kwa tabia ya wizi na hata ulevi, mtu anaanza kidogo kidogo na baadaye anakuwa mwizi au mlevi sugu kabisa. Kila tunachofanya kwenye maisha yetu ndiyo kipo hivyo. Tunaanza kidogo, kwa nia njema, lakini kiasi cha kufanya na hatuoni wakati gani wa kuacha. Tunapotea kabisa.

Wengi wamepotelea kwenye kazi au biashara zao, wanakuwa na mafanikio makubwa kwenye kazi au biashara hizo, lakini maeneo mengine ya maisha yao yanakuwa na changamoto kubwa. Hii inatokana na kukosa kiasi na kutokujua wakati sahihi wa kuacha.

SOMA; UKURASA WA 1017; Acha Kufanya Kazi, Anza Kuzalisha…

Wapo ambao wamepotezwa kabisa na kukimbizana na kila aina ya fursa, kwa sababu hawakuwa na kiasi katika kuchagua fursa, hawakujua ni wakati gani wakuacha kukimbizana na kila aina ya fursa na kuchagua fursa moja ambayo wataifanyia kazi kwa kina.

Kwenye kila unachofanya, jua kabisa kiasi cha kufanya na jua ni wakati gani wa kuacha na wakati upi wa kuendelea kufanya. Hili unapaswa kujua mwanzo kabisa unapoanza kufanya na litakusaidia kuwa na mafanikio yenye mlinganyo mzuri.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog