Neno mafanikio lina maana tofauti kwa watu tofauti. Lakini kwa ujumla wake mtu anafanikiwa pale anapofika pale anapotaka kufika na kupiga hatua ya kuwa bora zaidi leo kuliko alivyokuwa jana.

Kwenye shughuli zetu za kila siku, iwe ni kazi au biashara, tunahitaji kuwa na mafanikio pia. Shughuli tunazofanya kila siku, ndiyo zinachukua sehemu kubwa ya maisha yetu. Hivyo kama shughuli hizi hazitakuwa za mafanikio, maisha yetu hayatakuwa ya mafanikio pia.

Ili kuhakikisha kazi au biashara zetu zinakuwa na mafanikio makubwa, yapo mambo mawili muhimu ya kuzingatia;

MOJA; PENDA KILE UNACHOFANYA.

Maisha ni mafupi, muda wetu ni mfupi, hivyo kuchagua kufanya kitu chochote ambacho hukioendi, ni kuchagua kupoteza muda na maisha yetu. Kama nilivyokuambia hapo juu, kazi au biashara tunazofanya zinachukua sehemu kubwa ya maisha yetu. Hivyo ni muhimu sana ikawa kile unachofanya unakipenda.

Hakuna watu wenye maisha magumu kama wale ambao wanafanya kazi au biashara wasiyoipenda. Hata kama wanapata fedha nyingi kiasi gani, bado kuna utupu unaokuwa ndani yao.

Chagua kufanya kile unachopenda kweli, kile ambacho unaweza kufanya hata kama hakuna anayekulipa. Hichi kitakufanya upate utulivu wa moyo na hata kutengeneza kipato pia.

Lakini utajiuliza napataje fedha kwa kufanya ninachopenda? Na hapa ndipo tunaingia kwenye kitu cha pili muhimu kuzingatia.

MBILI; TOA THAMANI KWA WENGINE.

Dunia inaendeshwa na kitu kimoja; THAMANI.

Unaweza kupata chochote unachotaka, kama utawapa watu thamani zaidi. Hivyo kupitia kile unachofanya, angalia ni kwa jinsi gani unaweza kutoa thamani kwa wengine.

Angalia matatizo au changamoto ambazo watu wengine wanazo na ona unawezaje kuzitatua kupitia kile unachopenda kufanya. Hapa ndipo unapoleta hivi viwili pamoja na kuweza kutengeneza kazi au biashara yenye mafanikio makubwa kwako.

Kwenye kile unachopenda kufanya, angalia ni kwa namna gani unaongeza thamani kwa wengine. Angalia changamoto ipi unatatua, matatizo gani unayatolea ufumbuzi na kwa namna gani unayafanya maisha ya wengine kuwa bora zaidi.

Hayo ndiyo mambo mawili muhimu sana kuzingatia ili kazi au biashara unayofanya iwe na mafanikio makubwa kwako. Kupenda unachofanya na kutoa thamani kubwa kwa wengine kupitia unachofanya.

Swali kubwa wengi wanapenda kuuliza ni je kama ninachopenda kufanya hakuna anayeweza kunilipa nafanya nini? Jibu lake lipo wazi, angalia matatizo na changamoto ambazo watu wanazo, kisha angalia wewe unawezaje kuwasaidia kupitia kile unachopenda kufanya. Anza na watu na hutakosa cha kuwasaidia.

Nisisitize tena rafiki, muda wetu ni mfupi hivyo tuuthamini kwa kufanya vitu vinavyotuletea mafanikio makubwa kwetu na kuwasaidia wengine pia.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

http://www.amkamtanzania.com/kurasa