Moja ya vitu utakavyokazana navyo sana kwenye maisha, hasa pale unapotaka kuwa na mafanikio zaidi, ni kukutana na watu ambao wangekufaa kutokana na mahitaji yako, lakini watu hao wakawa hawakuamini.
Labda ni watu ambao wana fedha na wewe unazihitaji kwa ajili ya kuanzisha au kukuza biashara yako. Au ni watu wenye shida na uhitaji, na wewe una suluhisho la mahitaji yao. Au ni wateja wa biashara unayofanya, lakini hawakuamini na hivyo hawanunui kwako. Wanakuona na wanakuacha, wanaenda kule walipozoea.
Hali hii huwakatisha tamaa wengi, na kuona labda hawawezi kuaminika. Wengine wanakazana kujieleza ili waaminike. Lakini hakuna anayeaminika kwa maneno. Watu hawakuamini kwa sababu umewaambia niaminini mimi. Watu wanakuamini pale unapowapa sababu ya kufanya hivyo.

Na hapa tunakwenda kujifunza jinsi ya kuwapa watu sababu ya kukuamini. Na cha kwanza kabisa, matendo yanaongea kwa sauti kuliko maneno. Hivyo hatua ya kwanza kabisa ya kuaminika, ni kutoa yale matokeo ambayo mtu anayatarajia. Unayatoa matokeo hayo bila ya gharama yoyote kwa mtu unayetaka akuamini. Unahakikisha yeye hana cha kupoteza, na akishapata matokeo hayo, anakuwa na sababu ya kukuamini na kuchukua zile hatua unazotaka achukue.
SOMA; UKURASA WA 726; Kilichojificha Nyuma Ya Hofu Ya Kufanya Mambo Makubwa….
Wauza karanga wanalijua hili vizuri, akikutana na wewe atakuambia nauza karanga, ni karanga tamu kweli. Wewe hutaamini, una uhakika gani karanga hizo ni tamu, wakati hata muuzaji mwenyewe humjui. Basi yeye anakupa sababu ya kuamini anachosema. Anakuonjesha karanga kidogo, unaupata utamu kweli na unakuwa na sababu ya kununua.
Hivi ndivyo unavyopaswa kufanya kwenye kila jambo unalofanya kwenye maisha yako, ambalo unataka watu wakuamini. Wape watu sababu ya kukuamini, wape watu matokeo ambayo yatawafanya waone thamani iliyopo ndani yako.
Wakati mwingine utahitaji kufanya hivyo kwa gharama zako mwenyewe, lakini itakulipa zaidi baadaye.
Lazima nikukumbushe pia kwamba wapo utakaowapa sababu na bado wasikuamini, au wasichukue hatua. Sawa na wale wanaoonja karanga na hawanunui. Hao wasikukwamishe, endelea mbele kuwafikia watu sahihi kwako.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog