Hongera rafiki yangu kwa siku hii nzuri sana ya leo, siku njema, siku mpya, siku ambayo sisi wenyewe ndiyo tuna maamuzi inaanza na kuishaje.  Iwapo tutafanya yale yaliyo sahihi leo, siku ya leo itakwenda kuwa bora na ya tofauti kabisa kwetu.

Karibu kwenye kipengele cha makala za NYEUSI NA NYEUPE ambapo tunauangalia ukweli kama ulivyo, bila ya kuficha chochote au kuogopa mtu anaweza kujisikia vibaya. Sifa ya ukweli ni moja, ukweli utabaki kuwa ukweli iwe sisi tunapenda au hatupendi. Unaweza kukataa kwamba dunia haina nguvu ya mvutano, lakini ukirusha kitu juu lazima kitarudi chini. Unaweza kuelezea hilo utakavyo, lakini ukweli unabaki kuwa, vitu vinarudi chini kwa sababu dunia inavivuta.

Leo tunakwenda kuangalia eneo moja ambalo wengi hatupendi kuangalia. Hatupendi kujiangalia sisi wenyewe, tunapenda kuwaangalia wengine kwa makosa yao, na kuwasema kwa makosa yale. Lakini tunasahau kuangalia eneo moja muhimu sana, ambalo ni sisi wenyewe.

Hivi umewahi kuona hili, kwamba kuna mtu anakuwa analalamikia mtu ambaye yupo kwenye nafasi fulani, halafu yeye anapata nafasi kama ya mtu yule, na anafanya yale ambayo alikuwa anamlalamikia mwingine anayefanya? Kila kiongozi wa eneo fulani huwa wapo watu wanaomlalamikia kwa yale anayofanya. Cha kushangaza mmoja wa wale wanaomlalamikia akipata nafasi ya uongozi naye anafanya yale yale na analalamikiwa pia.

Huenda umewahi kukutana na watu ambao wanafanya vitu ambavyo vinakushangaza. Unajiuliza wanawezaje kufanya vile. Lakini kama wewe ungekuwa kwenye mazingira waliyo wao, usingekuwa na namna nyingine bali kufanya kama walivyofanya wao.

Hivyo ninachotaka tujikumbushe hapa rafiki yangu ni kimoja, kabla ya kusema, kulaumu au kulalamika juu ya kile ambacho wengine wanafanya, chukua dakika moja na jiulize, JE KAMA INGEKUWA NI WEWE UNGEFANYA NINI? Usikimbilie kutoa maneno yako kabla hujajiuliza na kujipa majibu ya swali hilo muhimu.

Achana

Na ukishapata majibu ya swali hilo, siyo mwisho, bali ni mwanzo. Sasa unachohitaji kufanya ni kutenda kile ambacho ungekitenda kwa nafasi ya yule unayeona hafanyi kwa usahihi. Kifanye kwa ngazi yako, hata kama ni ngazi ndogo, wewe fanya, fanya kuonesha mfano, fanya ujue kwa nini wengine hawafanyi.

Ninakutaka ufanye kwa sababu kuongea ni rahisi, kila mtu anaweza kuongea, anaweza kulaumu na anaweza kulalamika. Lakini wale wenye uwezo wa kuchukua hatua, ni wachache mno, na hawa ndiyo wanaopiga hatua kwenye kila hatua ya maisha yao.

Sasa zoezi tunalofanya leo, ni la kukuondoa wewe kwenye kundi la wasemaji, na kukuweka kwenye kundi la wafanyaji. Kwa sababu wafanyaji ndiyo wanaopata manufaa, huku wasemaji wakiishia kuwa wasemaji;

Ili tuelewane vizuri, labda nikupe mifano, uone namna gani unapaswa kufanya.

Kuna kiongozi ambaye unaona anayofanya siyo sahihi, badala ya kulalamika na kusema kipi sahihi angefanya, fanya kilicho sahihi wewe kwenye uongozi wako. Kwenye eneo lako la kazi, biashara na hata kwenye familia, una nafasi za kuongoza wengine na hata kujiongoza wewe mwenyewe. Hebu fanya kile ambacho unaona kiongozi unayetaka kumlalamikia hafanyi. Itakufanya wewe kuwa bora zaidi.

SOMA; ONGEA NA KOCHA; Mapenzi, Hasira, Kujitoa Na Kupambana, Neno Langu Kwa Wale Walionasa.

Kuna mtu umeona amepata fedha nyingi halafu anazitumia vibaya, unaanza kuwa na maoni yako kwamba yule angepaswa kufanya hivi au vile. Hebu yaweke hayo maoni yako kiporo, halafu fanya kile ambacho unafikiri anayechezea fedha zake angepaswa kufanya. Kwa kiasi kidogo cha fedha ulichonacho, hebu jibane uweke akiba, uwekeze na mengine muhimu. Na vipi kama utaongeza kipato chako zaidi?

Labda kuna mtu unamwona ni tajiri, ana uwezo mkubwa kifedha ila amekuwa hawasaidii wenye uhitaji. Unaona kila mtu anasema fulani angepaswa kuwasaidia watu, hizo fedha anapoteza kwenye mambo yasiyo muhimu, angesaidia watu zingekuwa na maana zaidi. Wewe hebu kaa kimya, halafu anza wewe kusaidia. Hata kama kipato chako ni kidogo kiasi gani, wapo watu ambao unaweza kuwasaidia, hebu anza kuwasaidia wewe. Kwa sababu kama kwenye elfu kumi huwezi kumsaidia mtu elfu moja, usifikiri kwenye milioni kumi utaweza kumsaidia mtu elfu kumi.

Chochote unachoona wengine hawafanyi kwa usahihi, anza kukifanya wewe kwa usahihi. Hata kama kila mtu anasema, wewe kaa kimya, anza kufanya. Kwa kufanya utajifunza mengi na utakuwa bora zaidi. Utajifunza kwa nini wale unaowalalamikia hawafanyi, kwa sababu mara nyingi kufanya ni kugumu. Pia zoezi hili litakuokolea muda wako, badala ya kuupoteza kulalamika na kulaumu, ambako hakukusaidii lolote, utautumia kufanya kitu ambacho kitakuwa bora zaidi kwako.

Hata kama unapata msukumo kiasi gani ndani yako ya kuwasema wale ambao unaona hawafanyi kwa usahihi, usifanye hivyo, wewe chukua hatua.

MUHIMU; Hii haimaanishi kwamba hupaswi kuwasahihisha watu, unapaswa kufanya hivyo, kama unaweza kumfikia mtu na kuongea naye ana kwa ana, kuhusiana na kile anachofanya na kisha ukamshauri njia bora kabisa ya kufanya, ambayo wewe pia umeshafanya. Lakini wale unaowaona kwa mbali, wale unaoona tu wanafanya na huwezi kuwafikia na kuongea nao, nakushauri funga mdomo wako na fanya.

Mwanafalsafa Socrates amewahi kusema kila mtu anapigana vita yake, kuwa na huruma kwa watu, hujui nini wanapitia mpaka wakafanya kile wanachofanya. Ukifanyia kazi zoezi hili, utakuwa umesogea karibu kabisa na kile ambacho watu wanapitia, au kinachowazuia kufanya kile walichotegemewa kufanya.

Kaa kimya, jiulize je mimi ningefanya nini? Kisha fanya. Kuna ugumu kwenye hilo?

Usomaji

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Kama umejifunza kupitia makala hii karibu tujifunze zaidi kupitia KISIMA CHA MAARIFA, ambapo utaingia kwenye kundi la wasap na kupata mafunzo kila siku. Bonyeza maandishi haya kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog