Watu wengi wanaotaka kubadili maisha yao na wafanikiwe huwa wanashindwa, kila hatua wanazochukua hawapati matokeo ambayo walikuwa wanatarajia. Mwishowe wanaona kama wao hawawezi na hivyo kukata tamaa.

Kinachowasababisha washindwe kupata matokeo wanayotaka, ni kwa sababu mabadiliko wanayoyafanya kwenye maisha yao siyo sahihi. Wengi wamekuwa wanajaribu kubadili nje wakati ndani kupo vile vile. Ni sawa na kutaka kubadili matunda ya mti kwa kukata matawi na kuliacha shina kama lilivyo, haileti matokeo unayotaka.

wp-image--1427239600

Njia sahihi ya kuleta mabadiliko ya kweli na yadumuyo kwenye maisha yako na kuweza kufanikiwa lazima iguse maeneo haya matatu muhimu.

Moja; Fikra.

Jinsi unavyofikiri inachangia sana aina ya maisha unayokuwa nayo na matokeo unayoyapata. Kile unachofikiria kwa muda mrefu, ndiyo kinachotokea kwenye maisha yako.

Fikra zako ni eneo la kwanza la kufanyia kazi kwenye mabadiliko unayotaka kuleta kwenye maisha yako. Lazima uanze kwa kubadili fikra zako, badili namna unavyofikiri.

Huwezi kuwa na maisha mapya kama bado unafikiri kama ulivyokuwa ukifikiri zamani. Zipo fikra zinazokurudisha nyuma, zipo fikra hasi na zote hizo zinakuwa kikwazo kwako kupiga hatua.

Lazima uanze na fikra zako, uhakikishe ni fikra sahihi kwako kuweza kupiga hatua na kufanikiwa.

Mbili; Kuwa.

Jinsi unavyofikiri, ndivyo unavyokuwa. Lakini muhimu zaidi ni kwamba, unahitaji kuwa kabla hujapata unachotaka. Inabidi uvae viatu vya kile unachotaka kabla hujakipata.

Mabadiliko ya kweli kwenye maisha, yanatokea pale unapobadili kabisa mfumo wako wa maisha. Unahitaji kuishi kama vile wanavyoishi wale ambao wana kile unachotaka.

Unafanikiwa kwenye maisha kwa kuishi jinsi ambavyo watu wamefanikiwa wanaishi. Wengi hufanya hili kinyume, wakiamini kwamba wakishafanikiwa basi ndiyo wanaweza kuishi kama waliofanikiwa. Unakuwa kwanza ndiyo unapata matokeo unayotaka.

SOMA; UKURASA WA 966; Kitu Pekee Unachomiliki Kwenye Maisha Yako, Unachopaswa Kukitunza Sana…

Tatu; Zalisha

Kama huzalishi, huwezi kubadilika, huwezi kufika kule unakotaka kufika. Unaweza kuwa na mipango mikubwa utakavyo, unaweza kuwa na maandalizi ya kutosha kabisa lakini kama hutakaa chini, uchukue hatua ambazo zitazalisha matokeo, basi jua hakuna chochote kinachoweza kubadili maisha yako.

Mengine yote unayoyafanya ili kubadilika au kufanikiwa yanachangia kwa asilimia 10 kwenye mabadiliko na mafanikio yako. Uzalishaji unachangia kwa asilimia 90.

Ni muhimu sana uzalishe, ni muhimu sana uchukue hatua ambazo zitaleta yale matokeo unayoyatarajia. Mwanzoni inaweza kuwa vigumu kwako kuchukua hatua, lakini kadiri unavyochukua hatua, utajifunza na kuwa bora zaidi.

Fikiri, kuwa, zalisha ni maeneo matatu muhimu ya kufanyia kazi ili kuweza kupata mabadiliko na mafanikio ya kweli kwenye maisha.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog