Very little is needed to make a happy life; it is all within yourself, in your way of thinking. – Marcus Aurelius

Hongera mwanamafanikio kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni nafasi nzuri na ya kipekee kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Msingi wetu wa maisha ya mafanikio ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA ambapo tunakwenda kufanya nakubwa leo na kila siku ya maisha yetu.

Asubuhi ya leo tutafakari MAHITAJI YA FURAHA NI MACHACHE…
Moja ya eneo ambalo wengi wamekuwa wanapotea ni kwenye kutafuta furaha.
Watu wamekuwa wakihangaika kupata vitu vingi wakiamini vinakuja na furaha.
Wanapata vitu hivyo lakini furaha wanaikosa.

Ni muhimu tukajikumbusha kwamba, mahitaji ya furaha ni machache, na yapo ndani ya kila mmoja wetu, yanaanzia ndani ya fikra zetu.
Popote ulipo, chochote unachofanya na chochote ulichonacho, unapaswa kuwa na furaha.
Kama huna furaha, siyo kwa sababu kuna kitu unakosa, ila kuna kosa unafanya kwenye maisha yako.

Hivi kama una afya njema na unaweza kufanya shughuli zako, na wakati wapo wenzako wanaumwa na wamelala kitandani, una nini cha kukusababisha ukose furaha?
Na kama unaumwa na umelala kitandani, jua kuna wenzako wanakufa na hata sasa kuna mtu anakufa, ila wewe upo hai, kwa nini ukose furaha?

Chanzo kikuu cha furaha kwenye maisha yetu ni sisi wenyewe. Ukishaanza kukimbiza vitu kwa mategemeo ya kupata furaha, umeshapoteza.

Tukawe na siku bora leo, siku ya furaha bila ya kujali tuna nini au tunakosa nini.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kurasa