Kitu pekee ambacho tuna uhakika nacho kwenye maisha ni kwamba hakuna kitu chenye uhakika. Yale maisha ambayo tumekuwa tunadanganywa kwamba ukifanya vitu fulani basi utakuwa na uhakika wa maisha, hayana uhalisia katika zama hizi.

Tunaamini kwamba kuna watu wenye majibu yote na majibu sahihi, lakini ukweli ni kwamba hakuna mtu mwenye majibu yote na majibu sahihi. Kila mtu anakazana kufanya akiwa hana uhakika.

Hii ni kusema kwamba, kila jambo tunalofanya kwenye maisha yetu, lina hatari. Lakini sisi binadamu huwa tunapenda kuepuka hatari, na hii inawapelekea wengi kushindwa kufikia ndoto za maisha yao.

Kuishi kwenyewe ni hatari, mambo mengi tunayokutana nayo kwenye maisha yetu yana hatari kubwa ya kumaliza kabisa maisha yetu. Lakini tunayafanya kwa sababu hatuna namna nyingine. Kwa mfano kusafiri kuna hatari ya kupata ajali na kufa, lakini tunasafiri kwa sababu hatuna namna nyingine.

Hapa ndipo mwandishi Bill Treasurer alipochukua hatua ya kutuandikia kitabu hichi cha RIGHT RISK, akituambia kwamba, zipo hatari sahihi kwetu kuchukua ili kufanikiwa. Kupitia kitabu hichi, Bill anatupa msingi muhimu wa kuzielewa hali za hatari, na hatua za kuchukua ili kuweza kuchukua hatari sahihi na kunufaika nazo.

right risk

Karibu tujifunze kupitia uchambuzi huu ili tuweze kujua hatari sahihi kwetu na kuweza kuchukua hatua ili kufanikiwa.

 1. Hatuwezi kuepuka hatari kwenye maisha yetu. Tunaweza kukazana sana kuondokana na hatari kwenye maisha yetu, lakini ukweli ni kwamba, hatuwezi kuepuka kabisa hatari kwenye maisha yetu. Tunachoweza ni kuhamisha hatari au kuichelewesha. Lakini kila jambo tunalofanya kwenye maisha lina hatari ya kushindwa au kutuumiza. Hivyo ni muhimu mtu uchague hatari zipi unazoweza kuzichukua kwenye maisha yako.
 2. Hatari sahihi kuchukua zinatusaidia kufikiri kwa kina na kufanya maamuzi sahihi. Kadiri maamuzi yanavyokuwa muhimu na yakawa na hatari, ndivyo tunavyokuwa makini katika kuyafanya. Bila ya hatari, watu wasingefanya maamuzi na maisha yasingekuwa na maana kubwa kuyaishi. Ila uwepo wa hatari, unatusaidia kufanya maamuzi sahihi kwenye maisha yetu.
 3. Zipo hatua mbili za kuchukua pale unapokuwa kwenye hali ya hatari.

Moja ni kufanya kitu, kuchukua hatua kwa kile ambacho unapitia.

Mbili ni kutokufanya kitu, kutokuchukua hatua yoyote na kuacha mambo yaende kama yanavyoenda.

Hatua zote hizi mbili zina hatari, ukifanya kitu unaweza kupata matokeo mabaya zaidi na usipofanya kitu unaweza kukosa fursa nzuri zaidi.

 1. Hatari siyo sawa kwa watu wote. Mtu anaweza kuchukua hatari eneo fulani wewe ukamshangaa, ukaona kwa nini anafanya jambo la aina hiyo. huenda hatari unazochukua wewe watu wanakushangaa. Hii ndiyo sababu kwenye kuchukua hatari, inabidi tuzungumzie hatari sahihi kwa mtu kuchukua, kwa sababu hatari zote hazilingani kwa watu wote. Hatari sahihi kwako inaweza isiwe sahihi kwa mtu mwingine. Hivyo kuwatumia wengine kama kipimo cha usahihi wa hatari unayochukua, siyo njia sahihi.
 2. Dunia ya sasa iliyojaa kelele, inafanya uchukuaji wa hatari kuwa mgumu zaidi. Tunaishi kwenye dunia ambayo mawasiliano ni masaa 24 kwa siku, siku saba za wiki na siku 365 za mwaka. Mawasiliano haya yaliyopitiliza yanafanya ufanyaji wa maamuzi kuwa mgumu kwa sababu kila unachotaka kufanya, wapo ambao watakuambia ni hatari kubwa zaidi. Lazima ujipe nafasi ya kuchambua hatari kwa umakini ili kuweza kuchukua hatua.
 3. Kukosa kitu cha kufanya kunatusukuma kuchukua hali za hatari. Sisi binadamu hatupendi kukaa bila ya kitu cha kufanya. Kitu kigumu sana kwetu kufanya ni kukaa mahali na kutulia. Ndiyo maana watu hata wakipata kile wanachotaka, bado wanakuwa na msukumo wa kuchukua hatua ambazo zinaweza kuwafanya wapoteze walichopata. Ni muhimu kujua hili ili kujua kichocheo cha wewe kuchukua hatari sahihi.
 4. Usisubiri hatari isukumwe kwako, bali wewe iendee hatari. Tunaweza kuwagawa watu kwenye makundi mawili, kundi la kwanza ni wale wanaoifuata hatari, wale wanaochukua maamuzi ya hatari kabla hata hawajalazimishwa kufanya hivyo. Hawa huwa wananufaika na maamuzi hayo na kupiga hatua. Kundi la pili ni wale ambao wanaogopa kuchukua maamuzi ya hatari na kusubiri mpaka wasukumwe kuchukua maamuzi hayo. Hawa ni wale wanaosubiri mpaka inafika hatua hakuna namna nyingine bali kufanya. Hawa huwa hawanufaiki na hatari wanazochukua.
 5. Kuna njia sahihi na njia ambayo siyo sahihi ya kuchukua hatari. Njia ambayo siyo sahihi inaweza isipelekee kushindwa au kuleta maumivu, lakini mara zote huleta majuto. Njia sahihi inaweza isilete mafanikio au usalama lakini huwa haina majuto. Hivyo ijue misingi sahihi ya kuchukua hatari ili uepuke kuwa na maisha ya majuto.
 6. Pamoja na kuwa tayari kuchukua hatari, kuna mambo ambayo yapo nje yetu yanayoathiri hatari tunazochukua ambayo lazima tuyazingatie. Mambo kama muda, fedha, ujuzi na hata msaada wa wengine, yanahitajika sana katika kuchukua hali za hatari.
 7. Kila mtu ni mtu wa kuchukua hatari na pia mtu wa kuepuka hatari. Yapo maeneo ya maisha yetu ambayo tupo tayari kuchukua hatua hata kama matokeo ni hatari kiasi gani. Pia yapo maeneo ambayo tunaogopa sana kuchukua hatua pale tunapoona kuna hatari ya kupata matokeo mabaya. Ni muhimu mtu uyajue maeneo haya, ili uweze kuyatumia vizuri. Kwa mfano kama kuna eneo unaogopa kuchukua hatari, jiulize kipi kinakusukuma kuchukua hatari kwenye maeneo mengine, kisha tumia kwenye maeneo hayo.
 8. Sifa nne za hatari sahihi kuchukua. Tumezungumzia sana kuhusu hatari sahihi, kwamba kila mtu ana hatari sahihi kwake. Je unaijuaje hatari sahihi kwako? Jibu ni hatari sahihi ina sifa hizi kuu nne;

Moja; Mapenzi; hatari sahihi ni kwa yale mambo ambayo unayapenda na kuyajali kweli.

Mbili; kusudi; hatari sahihi ni ile inayoendana na kusudi la maisha yako.

Tatu; misingi; hatari sahihi ni ile inayoendana na misingi unayoisimamia na kuiishi kwenye maisha yako.

Nne; nguvu ya kuchagua, hatari sahihi ni ile ambayo wewe unakuwa na nguvu ya kufanya maamuzi ambayo ni sahihi kwako.

SOMA; UCHAMBUZI WA KITABU; The 80/20 Principle (Siri Ya Kupata Matokeo Makubwa Kwa Kutumia Rasilimali Chache).

 1. Uchukuaji wa hatari sahihi ni kuchukua hatua. Unaweza kujipa moyo kwamba unaweza kuchukua hatari, lakini kama hutachukua hatua, hayo yote hayatakuwa na maana. Lazima ujue hatua sahihi za kuchukua na uzichukue.
 2. Utulivu ni muhimu katika kuchukua hatari. Pamoja na umuhimu wa kuchukua hatua kwenye hatari, utulivu ni muhimu sana. Watu wengi wamekuwa wanakimbilia kuchukua hatua bila kufikiri kwa kina na hiyo kupelekea kukuza hatari zaidi. Unahitaji kuwa na muda wa utulivu, muda wa kufikiri na kutafakari kwa kina kabla ya kuchukua hatari.
 3. Kabla hujaingia kwenye hatari, jijue wewe mwenyewe kwanza. Jua mambo gani unayasimamia na mambo gani unapingana nayo. Usikubali mazingira ya uharaka wa kuchukua hatari yakuzuie kuchukua hatua hiyo muhimu. Pia usichukue hatari kwa sababu wengine wanachukua hatari hiyo, kila mtu ana hatari sahihi kwake, hivyo jijue ili ujue hatari sahihi kwako. Utajijua kwa kuwa na muda wa kufikiri na kutafakari kwa kina kabla ya kuchukua hatari.
 4. Tengeneza eneo lako la utulivu, jipe muda wa kuwa mwenyewe, muda wa kufikiri na kutafakari kwa kina, kila siku na kwa muda fulani wa maisha yako. Usikubali kumpa kila mtu muda wako halafu ukajinyima wewe mwenyewe. Jipe muda wa kutosha na hii itakusaidia sana katika uchukuaji wa hatari kwenye maisha yako.
 5. Ishinde nguvu ya mazoea. Moja ya vitu vinavyokuzuia kuchukua hatari, ni hali ya mazoea, ambayo kila mmoja wetu anayo. Sheria ya mwendo ya Newton inasema kitu kitaendelea kuwa pale kilipo, iwe ni kwenye utulivu au mwendo mpaka pale nguvu itakapotumika kukitoa kitu kwenye hali hiyo. Wewe pia utaendelea kufanya kile ulichozoea kufanya mpaka pale utakapochukua juhudi za ziada kubadilika.
 6. Eneo la faraja ambalo kila mmoja wetu analo ndiyo kitu kikubwa kinachotuzuia kuchukua hatari. Kila mtu kuna kitu amesharidhika nacho, na hivyo kuchukua hatari ambayo inaweza kuvuruga kitu hicho inakuwa ngumu. Ndiyo maana watu wanaweza kuendelea kuwa kwenye ajira ambayo haiwalipi, kuliko kuchukua hatua, kwa sababu wameshazoea na kuridhika na kipato kidogo wanachopata.
 7. Itengeneze akili yako kuchukua hatari. Vile tulivyo, tumetengenezwa. Tumetengenezwa kutokana na elimu tuliyopata, malezi tuliyopewa na mazoea tuliyotengeneza. Matengenezo haya yamefanyika kwa kupandikiziwa na kujipandikizia imani ambazo tunaziishi kila siku. Ukitaka kuwa mtu unayechukua hatari sahihi, lazima ujitengeneze hivyo. Lazima ujijengee imani ambayo itakusukuma kuchukua hatua katika hali ya hatari. Imani hii unaweza kuijenga kwa kuchagua kukubali hali ya hatari na kuona ni sehemu ya maisha yako.
 8. Tengeneza sentensi ambayo utairudia mara kwa mara ili kujienga imani ya kuchukua hatua kwenye hatari. Ukishajua hatari sahihi kwako kuchukua, na ukajua kipi kinakuzia kuchukua hatari hiyo, unaweza kutengeneza kauli ambayo utarudia kujiambia mara kwa mara, inayokusukuma kuchukua hatua. Kila mara unajiambia kauli hii na unapokuwa kwenye hali ya kuchukua hatua ya hatari unajiambia kauli hiyo. hii inakusukuma kuchukua maamuzi sahihi.
 9. Kubali msukumo wa kuchukua hatari. Katika kuchukua hatari, kuna misukumo mbalimbali inayokujia. Kuna msukumo wa kutaka kufanya, huu ni msukumo wa yale matokeo ambayo unataka kuyapata. Pia upo msukumo wa wengine ambao wamefanya au wanafanya. Unapaswa kujua jinsi ya kuitumia misukumo hii kwa usahihi ili uweze kuchukua hatua sahihi kwenye maisha yako. Kadiri msukumo unavyokuwa mkubwa, ndivyo uchukuaji wa hatua unavyokuwa mkubwa.

Haya ni machache kati ya mengi unayoweza kujifunza kutoka kwenye kitabu hichi cha RIGHT RISK, pata na ujisomee kitabu hichi kwa sababu zama tunazoishi na zile tunazoziendea, hakuna kitu salama tena. Kila kitu ni hatari na kila kitu hakina uhakika. Uhakika pekee unaoweza kujitengenezea ni kuwa tayari kuchukua hatua wakati wowote.

Fanyia kazi haya ambayo umejifunza kwenye uchambuzi wa kitabu hiki ili uweze kuona matokeo bora kwenye maisha yako.

Usomaji

Kupata vitabu vya Kiswahili vya kujisomea ili kuweza kufanikiwa kwenye kazi, biashara na maisha kwa ujumla, tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

www.kisimachamaarifa.co.tz