Mafanikio ni kitu ambacho kila mtu anakitafuta, kila mtu anapenda kupiga hatua zaidi kutoka pale alipo sasa na kufika mbali zaidi.
Japo wengi hufikiria mafanikio kwa upande wa fedha na mali pekee, watu wanakazana kuhakikisha wanapiga hatua zaidi.
Pamoja na juhudi kubwa ambazo watu wanaweka, ambazo pia ni gharama ya mafanikio, ipo gharama nyingine ya mafanikio ambayo wengi hawaijui au kama wanaijua basi inawashinda kulipa.
Gharama hiyo ni MUDA, kila mafanikio yanahitaji muda, muda wa kutosha ili kweli kitu kiweze kusimama.

Lakini kama tunavyojua, hasa kwa zama hizi tunazoishi, watu wanataka kitu na wanakitaka sasa. Watu hawana tena subira, na wakiambiwa waweke muda wanaona kama wanachelewa.
Kila siku zipo fursa za uongo zinazojitokeza, fursa zinazowaahidi watu mafanikio makubwa kwa haraka, na wengi mno wanakimbilia fursa hizo. Wapo watu ambao wameshahangaika na fursa hizo kwa muda mrefu lakini hakuna mafanikio wamepata.
SOMA; UKURASA WA 1011; Matokeo Ya Kujiweka Wewe Mbele Ya Wengine…
Shika neno moja, kwamba gharama kuu ya mafanikio ni muda, kitu chochote kikubwa kinachokua muda kukua. Chochote unachoona wengine wamefanikisha, jua wameweka muda kuweza kufanikisha. Na mtu yeyote anapokuja kwako, akikuambia kuna njia ya mafanikio ya haraka, ambayo haihitaji muda, achana naye mara moja.
Kwa mafanikio yoyote unayotaka kwenye maisha yako, kuwa tayari kuweka muda, muda wa kutosha.
Kufanya mambo kuwa rahisi na kuepuka kurudi nyuma, amua nini unataka kwenye maisha yako, jua jinsi gani ya kukipata kisha weka muda kukipata.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog