Binadamu tunategemeana sana, tupo kwa ajili ya wengine na wengine wapo kwa ajili yetu. Hatuwezi kufanikiwa peke yetu, tunahitaji msaada na michango ya watu wengine pia.
Sasa hapa kwenye utegemezi wa wengine, ndipo wengi tunapopata changamoto, kwa sababu tunashindwa kupata kile ambacho tunataka kutoka kwa wengine. Inawezekana kuna mtu ungependa akusaidie kitu fulani, au akupe kitu fulani au akuamini na kukuruhusu kufanya kitu fulani, lakini watu wa aina hiyo wanakukatalia.
Unakuta kuna kitu muhimu sana unakihitaji, na yule ambaye angekuwezesha kukipata anakukatalia. Au ni wateja ambao unataka wakuamini na kununua kwako ila hawanunui. Mwajiri ulitaka akuamini na kukuajiri au kukuongezea mshahara lakini hafanyi hivyo.
Hapa ndipo wengi hukata tamaa na kuona labda hawana bahati, au wao hawakubaliki na hivyo hawawezi kufanikiwa.

Kwa upande wa pili wapo watu ambao wanaonekana kupata kila wanachotaka. Wakiomba kitu kwa wengine wanapewa, wanaaminika na kukubaliwa kufanya yale wanayotaka kufanya. Kwa nje unaweza kusema watu hawa wana bahati sana, au wanapendelewa.
Lakini ukweli ni kwamba, watu hao wanaijua siri moja muhimu ya kupata kile wanachotaka kutoka kwa wengine. Wanaijua tabia kuu ya binadamu ambayo ni ubinafsi, hivyo kama unataka kupata chochote kutoka kwa mtu, tumia tabia ya ubinafsi.
SOMA; UKURASA WA 953; Unachokichukia, Unakipa Nguvu Ya Kuendelea Kukusumbua…
Unachohitaji kufanya, ni kuanza kumpa mtu kitu, yaani kabla hujamwomba mtu kitu, wewe mpe kitu. Unapokuja kuomba, anajikuta akilazimika kukubali, kwa sababu anajua ulishampa kitu. Hata kama hakuwa tayari kukubali, nafsi yake itamsuta kwa kile ambacho ulishampa, atajiona ana wajibu wa kukupa kile ulichoomba.
Hata kwenye kuaminika, lazima ufanye kitu kwa wengine, ambacho kitawafanya wajenge imani juu yako. Hutaweza tu kuaminika kwa maneno, utaaminika kwa kile ambacho umewafanyia wengine.
Hivyo kabla hujaomba, kwanza toa kitu, fanya kitu kwa ajili ya wengine.
ANGALIZO; Njia hii ya kutoa kabla ya kuomba ina nguvu kubwa, ukiitumia vibaya inaweza kuleta madhara kwako. Hivyo unavyotoa, toa kweli, toa kwa nia ya kusaidia na usitoe kwa sababu unategemea kuomba au kupata kitu fulani. Japo hilo ndiyo litakalotokea, nia yako ikiwa ni kwa sababu tu ya kupata, watu watajua na watakuogopa kama ukoma.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog