Kama

Habari ya leo mpendwa rafiki na msomaji wa mtandao wa Amka Mtanzania? Ni matumaini yangu kuwa hujambo na unaendelea vizuri. Hongera sana rafiki kwa zawadi ya siku hii ya leo kwani kuamka salama ni ushindi mkubwa katika maisha yako hivyo tumia ushindi huo wa uhai kuacha alama siku hii ya leo kumbuka kuwa maisha ni muda. Kumbuka kuiendea siku hii ya leo kwa misingi yetu ya Amka Mtanzania ya nidhamu, uadilifu na kujituma.

Rafiki, napenda kutumia nafasi hii kukualika tena siku hii ya leo katika makala yetu ya leo ili tuweze kujifunza wote kwa pamoja yale mazuri niliyoweza kukuandalia siku hii ya leo. Kwa namna ya pekee rafiki yangu, nakusihi sana tusafiri pamoja hadi mwisho wa somo letu la leo ambapo leo tutakwenda kujifunza kitu pekee ambacho hakuna mtu anayeweza kukunyang’anya katika maisha yako je unajua ni kitu gani ? Karibu tujifunze.

Mpendwa msomaji, Kama kuna kitu  unapenda kufanya basi huwezi kukosa muda kukifanya kitu hiko. Kila mtu amepewa zawadi ya muda lakini wachache sana wanaojali na kuutumia muda wao vizuri kila siku. Muda ni kitu ambacho wewe mwenyewe unakimiliki lakini kwa bahati mbaya huwezi kuusimamisha muda na kuupeleka kama vile unavyotaka wewe.

 

Kitu pekee ambacho  hakuna mtu anayeweza kukunyang’anya katika maisha yako basi ni muda. Tunayo mifano mingi ya watu ambao waliweza kutumia muda wao vizuri licha ya kuwa kifungoni. Mwanafalsafa Seneca licha ya kuwa kifungoni lakini hakuna mtu aliyeweza kumnyang’anya muda wake hivyo aliendelea na kuandika licha ya kuwa kifungoni. Licha ya Nelson Mandela kukaa kifungoni miaka 27 lakini hakuna mtu aliyeweza kumnyang’anya muda wake wa kuendeleza harakati za ukombozi wa taifa lake.

SOMA; Huyu Ndiye Mtu Asiyeishiwa Sababu Katika Maisha Yake.

Unaweza kunyang’anywa vyote lakini hakuna mtu anayeweza kukunyang’anya muda wako. Hata mtu akufungie ndani, gerezani lakini ni ngumu na ni kitu ambacho hakiwezekani kukuibia muda wako. Hakuna mtu aliyefanikiwa kuibiwa muda wake na kulalamika kuwa fulani ameninyang’anya muda wangu.

Rafiki, Mali na vitu vyote ulivyonavyo unaweza kunyang’anywa lakini muda hakuna mtu anayeweza kukunyang’anya kumbe muda ni kitu cha thamani sana katika maisha kuliko vingine. Pale tu unapokufa na wewe unaondoka na muda wako lakini ukiwa hai hakuna atakayeweza kukunyang’anywa muda wako.

Ukiwa unaumwa, umelala au unafanya nini hakuna atakayeweza kukunyang’anya muda wako hata siku moja.  Kwahiyo, tunapolalamika juu ya muda tuanze kujiuliza hivi ni mara ngapi dunia inakunyang’anya vitu mbalimbali mpaka hapo ulipo sasa lakini dunia ilishawahi kukunyang’anya muda? Wengine wanaweza kusema wamenyang’anywa simu na vibaka lakini huwezi kumkuta mtu amelalamika kuwa amenyang’anywa muda wake.

Mpendwa msomaji, kama hakuna mtu anayekunyang’anya muda wako kokote pale duniani kwanini sasa unaweka sababu nyingi za kushindwa kufanya  yale muhimu katika maisha yako? shabaha yangu ni kwamba mtu anayelalamika amekosa muda wa kufanya kitu fulani jua kabisa hicho kitu siyo muhimu kwake. Popote pale ulipo kama umeamua kufanya kitu hakuna anayeweza kukuzuia.

SOMA; Vitu Viwili Unavyohitaji Ili Kazi Au Biashara Yako Iwe Na Mafanikio Makubwa.

Hatua ya kuchukua leo, muda ni zawadi ambayo haifananishwi na kitu chochote kile na hakuna mtu ambaye anaweza kukunyang’anya muda wako hivyo utumie vizuri muda wako na sababu za kutokufanya kwa sababu ya muda zifute kabisa katika maisha yako. Muda unao kama ukiamua kuutumia vizuri na kuupangilia vizuri kila dakika ya maisha yako.

Kwahiyo rafiki, maisha yetu ni muda na tusipotumia vizuri muda wetu tutaendelea kubaki watupu. Jaribu kufanya kitu chochote chanya ili uweze kuacha alama duniani, hakuna anayekuzuia ila wewe mwenyewe,kumbuka kuwa hakuna anayeweza kukunyang’anya muda wako hata siku moja.

Makala hii imeandikwa na Deogratius Kessy ambaye ni mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali, unaweza kuwasiliana naye kupitia namba 0717101505/0767101504 au kwa barua pepe deokessy.dk@gmail.com, kessydeo@mtaalamu.net  au unaweza kutembelea tovuti yake, www.mtaalamu.net/kessydeo ,www.actualizeyourdream.blogspot.com kwa kujifunza zaidi kila siku. Asante sana.