Ukiona sehemu kuna mlima mkali, jua pia utakutana na bonde kubwa katika eneo hilo. Na kadiri mlima unavyokuwa mrefu, ndivyo bonde pia linavyozidi kuwa kubwa. Hivi ndivyo dunia ilivyo, ndivyo sheria ya asili inafanya mambo yaende.

Hii pia ipo kwa watu, kadiri mtu anavyokuwa imara, ndivyo pia anavyokuwa dhaifu. Hii ina maana kwamba, wale watu ambao ni wakuu na wanaweza kufanya makubwa, pia wana madhaifu na mapungufu makubwa kuliko wengine.

Zawadi Kubwa

Sasa kwa bahati mbaya, tunaishi kwenye dunia ambayo watu wanakazana kutafuta madhaifu ya wengine, na kuyatumia kuwaangusha. Na kwa kuwa watu wenye mafanikio makubwa pia wanakuwa na madhaifu makubwa, wengi sana wamekuwa wanaangushwa na madhaifu yao.

Kingine kibaya zaidi ni kwamba watu hawapendi kukubali kwamba wana madhaifu. Hasa watu wanapokuwa juu, wanapokuwa wamefanikiwa, huamini kwamba wao hawana madhaifu, na ndiyo maana wamefanikiwa. Hata pale wengine wanapojaribu kuwaonesha madhaifu yao, huwa hawakubali. Hilo pia kinachangia kuwaangusha zaidi.

Hivyo cha kufanya, kwanza yajue madhaifu yako. Jua ni maeneo gani haupo imara, jua madhaifu yako ni yapi, jua maeneo gani haupo vizuri. Hii ni hatua ya kwanza kabisa katika kuhakikisha madhaifu yako hayawi kikwazo kwako au hayatumiki kukuangusha.

Hatua ya pili ni kuangalia namna ya kuzuia madhaifu hayo yasiwe kikwazo kwako. Elewa vizuri hapo, sijakuambia ukazane kuyafunika au kuyarekebisha, bali kuangalia namna gani hayawezi kuwa kikwazo kwako. Kama ni tabia mbaya basi jenga tabia nzuri, kama ni uwezo mdogo kwenye maeneo fulani ya kazi au biashara yako, basi zungukwa na wenye uwezo mkubwa kwenye maeneo hayo. Usikazane kuwa imara kwenye kila eneo, utaishia kuwa hovyo kwenye kila eneo.

SOMA; UKURASA WA 624; Hatua Iliyo Ngumu Zaidi Kwenye Safari Ya Mafanikio…

Mwisho kabisa, kubali pale wengine wanapokuonesha madhaifu yako. Usiwaone kama ni maadui au watu wanaotaka kukuangusha, badala yake pokea maoni na mrejesho wa wengine kwenye yale yanayofanya na chukua hatua kuhakikisha unakuwa bora zaidi.

Zingatia sana hili, unaweza usione madhara ya madhaifu yako kwa sasa kwa sababu hujapiga hatua kubwa, ila utakapopiga hatua kubwa, watu watatumia madhaifu hayo kukuangusha.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog