Moja ya kikwazo kikubwa kwa wengi kufanikiwa ni hofu. Ni rahisi sana kupanga mambo ambayo mtu atafanya, ni rahisi kukaa chini na kuweka malengo na mipango. Lakini inapofika kwenye utekelezaji, ndipo wengi hushindwa kuchukua hatua kwa sababu ya hofu.
Wengi hujiona bado hawajawa tayari, huona wanaweza kushindwa, watakataliwa au wataonekana vibaya kwa wengine. Kwa hofu hizi, wengi huona wasianze kwanza mpaka pale watakapokuwa na uhakika kwamba hayo wanayohofia hayatatokea.
Katika kuacha, hakuna kinachobadilika, na hata yale waliyokuwa wanahofia awali yakiondoka, yanakuja mengine makubwa zaidi ya kuhofia.
Ninachotaka kukukumbusha ni kwamba, hofu hazitaondoka na kuisha kabisa. Ukifanikiwa kumaliza hofu moja, zipo nyingine zinajitokeza. Ukitatua changamoto moja, nyingine zinajitokeza. Siyo kwamba kuna watu hawataki ufanikiwe, bali ndivyo dunia inavyoenda, ndivyo mambo yalivyo.
Hivyo basi, njia pekee ya kukabiliana na hofu, njia pekee ya kuishinda hofu ni kuitumia. Badala ya kuacha kufanya kwa sababu ya hofu, unaanza kusukumwa na hofu kwenye kufanya.
Unachofanya ni kuifuata hofu, chochote ambacho unahofia kufanya, basi hicho ndiyo unaanza kufanya. Kile ambacho unaona hujawa tayari kufanya, hicho ndiyo unaanza kukifanya.
SOMA; UKURASA WA 999; Unapoukaribia Ukweli, Hofu Inaongezeka…
Kwa njia hii utagundua mambo mawili makubwa;
Moja, mambo siyo mabaya kama ulivyokuwa unafikiri, hata yale uliyokuwa unahofia yatatokea, mengi hayatokei. Yale uliyokuwa unafikiri yatakuwa makubwa sana hayawi hivyo.
Mbili; una kila unachohitaji ili kuchukua hatua, na hata ambacho huna kinakuja chenyewe ukishaanza kufanya. Utaona namna gani dunia inakupa kile unachotaka unapoanza kufanya na kukataa kukata tamaa.
Hivyo rafiki yangu, usitegemee hofu kuondoka kabisa, na wala usikazane kuiondoa hofu kwenye maisha yako. Badala yake itumie, itumie hofu kama kiashiria cha wapi pa kuchukua hatua, kwa sababu kile unachohofia, ndiyo kikubwa na ukikifanya utafanikiwa zaidi.
Hofu itaendelea kuwepo, itumie kama ishara ya kuelekea kwenye mafanikio yako.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Ahsante sana Kocha,
Hakika nita itumia hofu kama kichocheo cha kuchukua hatua kuelekea kwenye mafanikio yangu
LikeLike
Karibu sana.
LikeLike