Habari za leo rafiki yangu?

Changamoto ni sehemu ya maisha yetu ya kila siku. Hakuna kitu kinachokuja kirahisi kwenye maisha, licha ya kuweka malengo na mipango mizuri kwenye maisha yetu, huwa zinajitokeza changamoto ambazo kwa wengi zimekuwa ndiyo mwisho wa safari yao ya mafanikio.

Lakini haiaswi kuwa hivyo, hupaswi kuzima ndoto zako kwa sababu ya changamoto unazokutana nazo. Badala yake unahitaji kuzitatua ili usonge mbele zaidi.

Katika kutatua changamoto, ndipo penye kazi kubwa zaidi, wengi hawajui njia zipi watumie kutatua changamoto zao, na hapo ndipo msaada wa ushauri unapokuwa unahitajika ili mtu ajue ni hatua zipi za kuchukua.

Hapa kwenye ushauri ndipo wengi zaidi wamekuwa wanakosea, wengi wanakazana kuchukua kila aina ya ushauri wanaoweza kupata, kwa kila anayeweza kutoa, lakini wanasahau sehemu moja muhimu ambayo wanaweza kupata ushauri bora kabisa kwa lolote wanalopitia.

Kwa ulimwengu wa sasa, wa mitandao ya kijamii na mawasiliano ya masaa 24 kwa siku na kwa dunia nzima, watu ni rahisi kuweka matatizo na changamoto zao kwenye mitandao ya kijamii wakiamini watapata ufumbuzi. Lakini hili limekuwa haliwapi matokeo mazuri.

Wengine wamekuwa wakikazana kuomba ushauri kwa watu mbalimbali, kuanzia wenye uzoefu na hata wasio na uzoefu. Wapo ambao wanapokea kila aina ya ushauri wanaoweza kupata na kuanza kuutumia kwenye matatizo na changamoto zao. Baadaye wanakuja kugundua kwamba ushauri waliopata haukuwa sahihi kwao.

Leo nataka nikuoneshe sehemu moja muhimu ambayo unaweza kupata ushauri bora kabisa wa hali yoyote unayopitia. Sehemu hii ukiweza kuitumia vizuri, utaweza kutatua matatizo na changamoto zako zote na kuwa na maisha bora.

Wengi wamekuwa hawaitumii sehemu hiyo kwa sababu hawajui kama ipi na hata wale wanaojua uwepo wake, hawaamini au hawapendi kuweka juhudi zinazohitajika ili kupata suluhisho wanalotaka.

Sehemu tunayokwenda kujifunza leo, ambayo unaweza kuitumia kutatua matatizo na changamoto zako zote ni akili yako.

Unaweza kuona ni rahisi na kitu cha kawaida kwako kujua, lakini nikuhakikishie kwamba huenda hujui, kwa sababu wengi wamekuwa hawajui. Wengi wamekuwa wanafikiri ukishalifikiria tatizo basi umeshatumia akili yako, na hapo ndipo wanapopotea.

Kwanza tuanze na sifa za akili yako;

Akili yako ni kitu ambacho kipo na wewe tangu unazaliwa mpaka sasa. Ni kitu ambacho kimetunza kumbukumbu zote tangu umeingia kwenye hii dunia. Kila kitu ambacho umewahi kufanya, kila kitu ambacho umewahi kukutana nacho, hakijapotea, kimehifadhiwa ndani ya akili yako.

Akili yako ina uwezo mkubwa sana wa kufikiri na kubuni mambo makubwa, ila ni kama tu itatumiwa, kama italazimishwa kufikiri kwa kina basi itakuja na majibu bora.

Lakini watu wengi wamekuwa wanafanya kosa moja kubwa, wamekuwa hawapendi kutesa akili zao. Wamekuwa wanakwepa kuiumiza akili kwa kuifikirisha kwa kina. Na hivyo wamekuwa wakishindwa kutumia akili zao katika kutatua matatizo na changamoto zao.

Akili yako una uwezo wa kukupa majibu kwa matatizo na changamoto zozote unazopitia. Akili yako inaweza kwenda ndani zaidi kwenye tatizo na ndani yako na kukuonesha ni hatua zipi unazoweza kuchukua. Lakini lipo sharti moja kwenye hili, lazima uilazimishe akili yako kufanya hayo. Haitafanya kirahisi kama haitalazimishwa.

Njia ya kuilazimisha akili yako ije na majibu na ikupe matokeo mazuri ni kuilazimisha kufikiri kwa kile unachotaka kutatua. Na ili kufanya hivyo unahitaji vitu vitatu, sehemu tulivu, kalamu na karatasi, ukiwa na kijitabu itapendeza zaidi.

Baada ya kuwa na viti hivi vitatu, unaweza kuanza kuilazimisha akili yako ikupe majibu bora kwa lolote unalotaka.

Kaa sehemu tulivu, fungua ukurasa mpya wa kijitabu chako, juu ya ukurasa huo andika swali au changamoto inayokusumbua kisha orodhesha namba moja mpaka ishirini. Kisha kaa pale na ilazimishe akili yako kuja na majibu ishiriki kuhusiana na tatizo au changamoto hiyo. Hakikisha una utulivu wa kutosha, usiwe hata na simu, na hakikisha huondoki mpaka upate majibu hayo 20.

Usijali kuhusu ubora wa majibu, usijali kuhusu kuwezekana au kutokuwezekana kwa jibu unalopata. Wewe orodhesha majibu 20 ya namna ya kutatua changamoto yako. Usijihukumu wala kujikosoa wakati wa kuorodhesha majibu hayo 20, hiyo ni kazi ya baadaye.

Ukiweza kuishikilia akili yako kwenye hali hiyo, lazima itakupa majibu. Itakupa majibu ambayo hujawahi kufikiri kabisa. Utaona fursa ambazo zimekuwa mbele yako mara zote ambazo hujawahi kuziona kabisa. unaweza ufikiri ni maajabu kumbe ni kitu ambacho kipo ndani yako.

Baada ya kupata majibu yako ishirini, sasa unaweza kuchambua moja moja na kuona lipi unaanza kulitekeleza na lipi bora zaidi.

Fanya zoezi hili mara kwa mara, itumie akili yako vizuri ili kupata matokeo bora kabisa. Usikimbilie kupelekea matatizo na changamoto zako kwa wengine kabla hujaanza na akili yako. Una hazina kubwa ndani yako, itumie.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Kama umejifunza kupitia makala hii karibu tujifunze zaidi kupitia KISIMA CHA MAARIFA, ambapo utaingia kwenye kundi la wasap na kupata mafunzo kila siku. Bonyeza maandishi haya kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog