True happiness is… to enjoy the present, without anxious dependence upon the future. – Lucius Annaeus Seneca

Hongera rafiki kwa siku hii nzuri sana ya leo.
Ni nafasi ya kipekee kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Msingi wetu wa maisha ya mafanikio ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA ambapo tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.

Asubuhi ya leo tutafakari FURAHA NI SASA, HAPO ULIPO…
Moja ya vitu ambavyo tumefundishwa kujidanganya ni kuisogeza furaha mbele.
Tangu tukiwa watoto, tumekuwa tunafundishwa kuwa na furaha baada ya matokeo fulani.
Mtoto ambaye hajaanza shule hufikiri atakuwa na furaha akianza shule.
Akianza shule furaha inasogozwa mbele, anafikiria atakuwa na furaha akimaliza shule, au akifaulu mtihani, au akitoka ngazi moja kwenda nyingine.
Akimaliza shule furaha inahamishiwa kwenye kupata kazi,
Akipata kazi furaha inahamishiwa kwenye kuongezewa kipato.
Akizoea kazi furaha inahamishiwa kwenye kustaafu.

Mtu anaishi miaka zaidi ya 60 hajawahi kuwa na furaha ya kudumu, zaidi ya hiyo furaha ya kutegemea kitu fulani kitakachotokea.
Ninachotaka tujikumbushe asubuhi hii ni kwamba, kama hapo ulipo sasa, huna furaha, kama unajiambia baada ya kitu fulani ndiyo utakuwa na furaha, jua wazi kwamba hata baada ya kitu hicho huwezi kuwa na furaha.

Furaha ni sasa, hapo ulipo kwa kile ulichonacho. Chochote cha ziada unachofikiri unahitaji unajidanganya. Na uongo huo utakugharibu maisha yako kama hutastuka haraka na kuchukua hatua.

Ishi maisha yako sasa, ishi kwa furaha sasa.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha