Muda ndiyo kitu pekee ambacho tunacho kwa uhaba na ukomo wa hali ya juu sana. ni kitu tunachohitaji sana, lakini hakuna namna ya kukiongeza. Ni masaa 24 ya siku, siku saba za wiki na wiki 52 za mwaka, hakuna zaidi ya hapo.

Lakini kuna nyakati kwenye maisha yetu, ambapo tunahitaji muda zaidi. Kuna maeneo ya maisha yetu tunahitaji muda zaidi. Lakini hakuna muda wa ziada kwenye siku zote. Na muda lazima uende, iwe tunautumia au la.

Ni katika nyakati na maeneo kama hayo tunajikuta kwenye msongo, tuna mengi ya kufanya na muda haututoshi. Kadiri tunavyokuwa na msogo wa kwa nini muda hautoshi, ndivyo tunavyozidi kuupoteza huo muda.

Muda Unaotumia

Njia bora kabisa ya kuhakikisha muda wetu tunautumia vizuri na kwa yale ambayo ni muhimu kwetu ni kupunguza yale tunayofanya na yanayochukua muda wetu.

Kila unachoruhusu kitumie muda wako, yaani unachofanya au kuvumilia kiendelee kwenye maisha yako, maana yake ni kipaumbele kwako. Ina maana kwamba katika vyote unavyoweza kufanya na vinavyohitaji kufanya vile ulivyochagua kufanya ndiyo muhimu zaidi.

SOMA; UKURASA WA 819; Umasikini Wa Muda…

Sasa kama umekuwa unafanya tu bila ya kufikiri kwa kina au kupanga, unajikuta ukiwa na vipaumbele ambavyo siyo vipaumbele. Unafanya mambo ambayo siyo muhimu sana, huku yale muhimu ukiyaacha.

Anza sasa kujihoji kwa kila unachofanya, je hichi ndiyo kitu muhimu kabisa kufanya kwa muda wangu? Na je kuna kitu kingine muhimu zaidi ya hichi ambacho ningeweza kuwa nakifanya muda huu?

Ukiwa mwaminifu kabisa kwako na ukiwa unajua nini unachotaka kwenye maisha yako, utaona mambo mengi sana unayofanya ambayo hayastahili kabisa muda wako.

Usifanye jambo lolote kwa sababu umezoea kufanya, bali fanya kwa sababu ndiyo muhimu kuliko mengine yote.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog