A sword never kills anybody; it is a tool in the killer’s hand. – Lucius Annaeus Seneca
Habari za asubuhi ya leo mwanamafanikio?
Hongera kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Leo tumepata nafasi nzuri na ya kipekee kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Msingi wetu wa maisha ya mafanikio ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA ambapo tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari UPANGA HAUUI, WATU NDIYO WANAUA…
Mara nyingi tumekuwa tunalaumu matokeo badala ya chanzo,
Kama mtu ameuawa kwa upanga basi tunasema upanga hi silaha hatari sana.
Kama watu wamekufa kwa ajali tunasema vyombo vya usafiri ni hatari mno.
Lakini ukweli ni kwamba, kitu kinachoua watu siyo silaha wala vyombo vya usafiri, badala yake kinachoua watu ni watu.
Mtu anatumia silaha kuumiza au kuua wengine.
Na hata vyombo vya usafiri, vinatengenezwa na watu, vinaendeshwa na watu na hata kufanyiwa marekebisho na watu.
Mpaka chombo kinahusika kwenye ajali, kuna namna mtu amefanya uzembe katika eneo fulani la kuhakikisha chombo na safari ipo salama.
Watu ndiyo wanaua watu, hivyo kama tunataka kuwa na maisha bora na salama kwa kila mmoja wetu, lazima watu wazingatie usalama wa wengine. Lazima kila mmoja wetu aanze kujali kuhusu maisha ya mwingine. Lazima tujue kama ambavyo sisi wenyewe tunapenda kuishi, ndivyo wengine pia wanavyopenda kuishi.
Watu wakishakuwa tayari kulinda maisha ya wengine, silaha hazina hatari yoyote.
Nakutakia siku njema ya leo, uende ukajali kuhusu maisha ya wengine.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha