Kitu kimoja ambacho kimekuwa kinawashangaza watu wengi kwenye mafanikio ni kwamba hakuna kitu cha nje kinachoonesha kuwatofautisha waliofanikiwa na walioshindwa.

Ukisema kwamba waliofanikiwa ni wa rangi fulani, utakuwa mwongo kwa sababu kwa kila rangi wapo watu wengi waliofanikiwa. Ukisema wenye elimu ndiyo wanafanikiwa zaidi unakutana na wasio na elimu kubwa ila wamefanikiwa.

Ukisema kutoka kwenye familia yenye uwezo ndiyo kunachangia kufanikiwa, utakutana na wengi waliotokea familia za kimasikini kabisa na wamefanikiwa. Hata ukisema biashara za aina fulani ndiyo zinaleta mafanikio, utakuta kwenye kila aina ya biashara wapo waliofanikiwa. Kadhalika kwenye kazi, dini, umri na kila tunachoweza kuona kwa nje.

Kwa hali hii ya kukosekana kwa tofauti ya nje kati ya waliofanikiwa na walioshindwa, wengi wanaishia kuamini kwamba huenda waliofanikiwa ni kwa bahati. Kwamba walijikuta tu wanakutana na mafanikio kwenye maisha yao.

Lakini hilo la bahati siyo kweli pia. Ukiwafuatilia kwa karibu watu wote waliofanikiwa, unagundua kuna vitu wanavifanya tofauti kabisa na wale ambao hawajafanikiwa. Ukiangalia mfumo wao wa maisha ni tofauti kabisa na wale ambao hawajafanikiwa.

Na kikubwa zaidi, yapo maamuzi mawili makuu ambayo waliofanikiwa wamekuwa wanayafanya kwenye maisha yao na kuyafanyia kazi, lakini ambao hawajafanikiwa hawayafanyi kabisa.

Maamuzi ya kwanza; kuamua nini hasa mtu anataka kwenye maisha yake.

Watu wengi wanaenda kwenye maisha wakiwa hawaelewi nini hasa wanataka, wanajaribu vitu vingi lakini hakuna kimoja au vichache ambavyo wanaamua kweli wanataka kuwa bora kwenye hivyo.

Kwa kukosa maamuzi hayo wanahangaika na kila aina ya kitu kinachopita mbele yao. Leo utawakuta na fursa hii, kesho unawakuta na fursa nyingine. Kwa kuwa watu hawa hawajui nini hasa wanachotaka, hawawezi kujua hata pale wanapokipata.

Na hasara kubwa zaidi, ni rahisi kwao kudanganyika na kuondolewa kwenye njia yoyote wanayoishika. Ni rahisi kushawishika na njia za mkato za kufanikiwa, ambazo huwa siyo sahihi lakini kwa kuwa hawana maamuzi wanaziamini au wanajidanganya wazijaribu.

Hivyo maamuzi ya kwanza muhimu kabisa, ni kuamua nini hasa unachotaka kwenye maisha yako.

Maamuzi ya pili; kuwa tayari kulipa gharama ili kupata kile unachotaka.

Baada ya mtu kuamua kitu gani hasa anataka kwenye maisha yake, hatua ya pili ni kuwa tayari kulipa gharama ili kupata kile mtu anachotaka.

Kila kitu kwenye maisha kina gharama zake, na tunapata chochote tunachopata kulingana na gharama tunayokuwa tayari kulipa.

Mafanikio makubwa yana gharama kubwa pia.

Yana gharama ya muda, itakuchukua muda mrefu mpaka kupata kile ambacho mtu unakitaka hasa. Na hii ndiyo gharama kubwa ambayo wengi hawapo tayari kulipa hasa kwa zama hizi. Zama tunazoishi ninza kasi, watu wanataka kitu na wanakitaka sasa. Hawana subira katika kupata kile wanachotaka. Na hili limewapoteza wengi zaidi.

Gharama nyingine kubwa ambayo mtu anapaswa kulipa ni kazi.

Mafanikio makubwa yanahitaji kazi kubwa pia. Unahitaji kufanya kazi zaidi ya wengine. Unahitaji kufanya kazi kwa muda mredu zaidi ya wengine na unahitaji kufanya kazi ngumu ambazo wengine hawataki kuzifanya.

Changamoto kubwa kwenye zama tunazoishi ni uongo unaosambaa kwa kasi kwamba zipo njia za mkato za kufanikiwa ambazo hazihitaji kazi. Kwamba kuna namna mtu anaweza kutumia akili tu akafanikiwa sana. Na ndiyo maana utaona wapo watu wengi wanaocheza kamari na michezo mingine ya kubahatisha. Hizi zote ni dalili za watu kuamini kwenye mafanikio bila ya kuweka kazi.

Rafiki, kama unataka mafanikio makubwa na ya kudumu kwenye maisha yako, fanya maamuzi haya mawili kama bado hujayafanya. Amua kipi hasa unataka kwenye maisha yako, kisha amua kulipa gharama ya kukipata. Hakuna kitu kisicho na gharama na gharama kubwa ni kazi na muda.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA www.kisimachamaarifa.co.tz/kujiandikisha

Kupata huduma za Ukocha; www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha

Kujiunga na Kundi la kusoma vitabu; www.amkamtanzania.com/kurasa

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog