Japokuwa tuna kazi na biashara nyingi tunazokimbizana nazo kila siku, hizi siyo kazi zetu kuu. Hizi ni kazi za ziada, baada ya kazi yetu kuu ambayo inaingia kwenye kile tunachokifanya.
Kazi yako kuu ni kuwa hai na kuwa mtu. Na ni kazi ngumu mno, ndiyo maana kila mtu anapambana na changamoto mbalimbali kwenye maisha yake. Changamoto zote tunazokutana nazo, zinatokana na kazi hii kuu ya kuwa hai na kuwa mtu.

Kuwa hai.
Bila ya uhai hakuna chochote unachoweza kufanya. Ukifa leo kila kitu ulichokuwa unafanya huwezi kufanya tena. Labda wengine wanaweza kuendelea, lakini wewe huwezi tena, ndiyo umefika tamati.
Hivyo kuhakikisha afya yako ipo vizuri wakati wote ni jukumu lako kuu la kwanza katika kazi yako ya kuwa hai. Lazima uhakikishe unajikinga na hatari zote zinazoweza kupelekea maisha yako kufika ukingoni kabla ya wakati wake.
Na muhimu zaidi, kula vizuri, fanya mazoezi na pata muda wa kupumzika. Haya matatu ukiyafanya vizuri, utaondokana na hatari nyingi kwenye maisha yako.
SOMA; UKURASA WA 1022; Acha Kujiua Kwa Kiu Huku Umezungukwa Na Maji Safi Na Salama…
Kuwa mtu.
Hapa duniani haupo peke yako, umezungukwa na watu wengine wengi. Na hata chochote unachofanya, unafanya na wengine na unafanya kwa ajili ya wengine.
Watu tunatofautiana sana, unayopenda wewe siyo wanayopenda wengine, juhudi unazoweka wewe siyo juhudi wanazoweka wengine. Wewe una mapungufu yako na wengine pia wana mapungufu yao.
Hivyo kazi kubwa kwako ni kuwa mtu, kuwachukulia watu kama walivyo, kuwakubali kwa yale mazuri wanayoyaleta na kuwavumilia kwa ule udhaifu walionao.
Kuwa mtu ni kazi kubwa kwa sababu wakati mwingine unahitajika kuwaamini wengine, licha ya kutokuwa na uhakika wa kutosha. Utu ndiyo unatuwezesha kushirikiana kwa pamoja na kuweza kufanya makubwa sana.
Kuwa hai na kuwa watu ndiyo kazi yetu kuu na ya kudumu kwa kipindi ambacho tupo hai hapa duniani. Tusiiache kazi hii kama kweli tunataka maisha bora na yenye mafanikio.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog