Uwekezaji wa rasilimali ardhi na majengo unazidi kubadili mwonekano wa nchi yetu tofauti na wakati uliopita, idadi kubwa ya watu inaongezeka kila siku na kuwa kimbilio mbadala tofauti na uwekezaji waliokuwa wakiufanya hapo awali. Uwekezaji wa zama za leo unahitaji kuwa mtu wa kujiridhisha na kuongeza umakini kabla hujafanya maamuzi ya kuwekeza popote kutokana na kutotabirika kwa hali tofauti za kiuchumi.  Uwekezaji huu umekuwa kivutio na kimbilio la wengi kutokana na uwezo wake wa kuongeza thamani na kuhimili mitikisiko mbalimbali ya kiuchumi tofauti na uwekezaji mwingine.

Chukulia umemiliki ardhi kwa matumizi ya kilimo fulani lakini kwa bahati mbaya ukapata hasara kwenye mazao uliyozalisha, ukweli utahuzunika sana, lakini kwa upande mwingine ardhi hiyo thamani yake itakuwa inaongezeka, vivyo hivyo hata kwenye majengo, unaweza ukatetereka kwenye mapato wakati wa hali ngumu ya kiuchumi lakini kumbuka kuwa ardhi yako na mjengo wako inazidi kuongezeka thamani yake bila kujali hali ya uchumi iliyopo kwa wakati huo. Usiwe mtumwa kwenye nchi yako, miliki ardhi sasa kwa kuwa ni mali na mtaji wa uhakika wa kuanza kufanya chochote unachoweza kama utaitumia kwa usahihi. Itumie ardhi kama mtaji wa kukutoa kwenye umaskini na kukupeleka kwenye uhuru wa kifedha.

majengo 39

Uhitaji mkubwa wa ardhi kwa matumizi mbalimbali ya kimaendeleo umekuwa chanzo cha mapato kwa walio wengi kutokana na kuwa ardhi ni mali. Lakini kuna idadi kubwa ya watu wameshindwa kumiliki ardhi kutokana na kushindwa kumudu gharama ambazo zimekuwa zikiongezeka kadri muda unavyo songa mbele. Usikate tamaa, bado unazo sababu nyingi za wewe kupata sehemu ya ardhi kwenye nchi yako. Leo napenda kukupa baadhi ya mambo yanayo sababisha utofauti wa gharama za viwanja.

Kiwango Cha Maendeleo Kwenye Eneo.

Viwango tofauti vya maendeleo baina ya sehemu moja na nyingine hutumika kama kipimo cha thamani ya viwanja kwenye eneo husika. Thamani ya ardhi huongezeka kadri kiwango cha maendeleo kinavyo ongezeka kwenye eneo husika. Maeneo yenye viwango vikubwa vya maendeleo huwa na gharama kubwa za viwanja tofauti na maeneo yenye maendeleo hafifu. Gharama hizi husababishwa na mzunguko mkubwa wa watu wengi kwenye eneo hilo hali inayosababisha uhitaji kuwa mkubwa tofauti na upatikanaji, uhitaji huu ni matokeo ya kuwa kivutio kwa matumizi mbalimbali ya makazi, biashara, viwanda na huduma za jamii.  Maeneo yenye maendeleo hafifu huwa na viwanja vya gharama nafuu zaidi ili kuwavutia watu wengi tofauti na maeneo yenye maendeleo makubwa ambayo gharama zake huwa kubwa.

Ujazo Halisi Wa Kiwanja.

Ardhi ni rasilimali ambayo inapimika kwa njia ya vipimo mbalimbali kwa yeyote anayehitaji kufanya hivyo. Kiwango halisi cha ukubwa au ujazo wa kiwanja husababisha kutofautiana kwa gharama kulingana na utofauti wa ujazo kati ya kiwanja kimoja na kingine. Kwa maeneo yaliyopimwa na kupangiliwa vizuri kila kiwanja huwa na ujazo unaofahamika na wakati mwingine huwa ni kipimo cha gharama husika kwa kila kiwanja, pia kwa maeneo yasiyopimwa njia za asili hutumika kupima ukubwa wa maeneo yao kama kipimo cha gharama ya eneo hilo. Ni muhimu sana ukajitathmini uwezo wako wa kifedha ili uweze kupata kipande cha ardhi ambacho una uwezo wa kukitumia na kukiendeleza kwa namna ambavyo umejipanga. Usiogope kununua viwanja vilivyopimwa kwa kuhofia gharama kuwa kubwa bali unapaswa kufahamu kuwa viwanja hivyo hutofautiana gharama kutokana na ujazo wake, vipo vya ujazo wa juu, ujazo wa kati na ujazo wa chini ili kutoa nafasi kwa watu wenye viwango tofauti vya kimapato.

SOMA; Hivi Ndivyo Unavyoweza Kukamilisha Ujenzi Kwenye Nyakati Ngumu Kiuchumi.

Mwonekano, Matumizi Na Umbo La Kiwanja.

Mazingira na mwonekano halisi wa viwanja husababisha kuwa na mvuto au kutokuwa na mvuto miongoni mwa baadhi ya watu wanao hitaji viwanja. Umbo halisi la kiwanja husababisha kuwa na mvuto au kutokuwa na mvuto kwa baadhi ya watu, viwanja vyenye maumbo ya mraba na mstatili huwa na mvuto mkubwa  sana tofauti na maumbo ya trapeza, msambamba, duara, pembe tatu na mengineyo. Pia matumizi tofauti ya viwanja husababisha utofauti wa gharama kutokana na kiwango halisi cha uhitaji wake kwenye soko, viwanja vya matumizi ya biashara na makazi huwa na uhitaji mkubwa sana tofauti na viwanja vya matumizi ya huduma za jamii na viwanda. Viwanja vilivyo kwenye muunganiko au kwenye kona za barabara huwa na mvuto zaidi tofauti na viwanja vilivyo nje ya muunganiko wa barabara na njia za mawasiliano. Maeneo tambarare yana mvuto mkubwa sana tofauti na maeneo yenye mabonde na milima kwa viwango tofauti. Kwa ujumla maeneo yenye mvuto na muonekano mzuri huwa na gharama kubwa tofauti na maeneo yenye mvuto hafifu kwa kuwa huwa na athari kwa chochote unacho kwenda kukifanyia kazi kwenye hicho kiwanja ikiwemo ubunifu na usanifu wa ramani.

Viwango Vya Upatikanaji Wa Huduma Za Jamii.

Kiwango halisi cha maendeleo ya huduma za jamii huwa ni kipimo kinacho ongeza au kufifisha thamani ya maeneo hayo, maeneo yenye uhakika wa upatikanaji wa huduma za jamii huwa na thamani kubwa tofauti na maeneo yenye upungufu au ukosefu wa huduma za jamii. Upatikanaji wa huduma bora za jamii hufanya jamii hiyo kuweza kuishi maisha yenye unafuu na kwa kujiamini katika kujiletea maendeleo yao binafsi na kwa jamii yetu yote tofauti na maeneo yenye upungufu au ukosefu wa huduma muhimu za kibinadamu. Maeneo yenye umeme, maji, hospitali, hoteli, shule, taasisi za fedha, kumbi za starehe, migahawa na vituo vya afya huwa ni kimbilio kwa watu wengi katika kupambana na hali zao za kijamii na kiuchumi. Ni muhimu sana kwa mamlaka husika kuhakikisha zinakwenda sambamba na kasi ya maendeleo na uhitaji mkubwa wa huduma hizo kwa watu wake ili kuwawezesha kujifanyia shughuli za kimaendeleo kwa gharama nafuu na kufurahia maisha.

Uwepo Na Ubora Wa Miundombinu.

Maeneo yenye hali nzuri ya hewa, mifumo mizuri ya barabara, mawasiliano, nishati mbalimbali, vivuko vya kuaminika, maji safi na maji taka, mazingira bora ya ukusanyaji taka ngumu na bila kusahau mifumo bora ya ulinzi na usalama huwa ni vivutio vikubwa kwa watu kufanya maendeleo makubwa na kwa haraka zaidi tofauti na maeneo yenye ukosefu  wa miundombinu hiyo. Mara nyingi mjadala mkubwa huwa ni kipi kitangulie kati ya miundombinu au watu kwenye uendelezaji wa maeneo mapya. Je miundombinu ipelekwe kwa ajili ya kuvutia na kupokea watu ili wafanye maendeleo au watu watangulie halafu wasubiri miundombinu ambayo utekelezaji wake unategemea vipaumbele vya sera za wakati huo. Uwepo wa miundombinu bora husababisha gharama za viwanja kuwa kubwa tofauti na maeneo yenye upungufu wa miundombinu. Kupanda kwa gharama hizi ni kutokana na kupata uhakika kuwa kile unachokwenda kuwekeza kitafanikiwa kwa wakati na gharama za maisha na uzalishaji zitakuwa nafuu zaidi tofauti na maeneo yenye upungufu wa miundombinu.

Tafakari yako kuhusu Makala hizi ni muhimu sana…..!!!! maoni na maswali yako ni mambo ambayo nayazingatia sana. Usisite kuwasiliana nami endapo dhamira yako itakusukuma kufanya hivyo. Karibu sana.

Tuendelee kuwa pamoja kupitia AMKA MTANZANIA tufike kwenye kilele cha mafanikio, pia endelea kufuatilia makala zijazo ili ujifunze zaidi.

Mwandishi wa makala hii ni mwanataaluma wa ujenzi.

Anapatikana kwa: Simu: +255 685 729 888

Baruapepe: kimbenickas@yahoo.com