Anger, if not restrained, is frequently more hurtful to us than the injury that provokes it. – Lucius Annaeus Seneca

Hongera rafiki yangu kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni nafasi bora na ya kipekee kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Msingi wetu wa maisha ya mafanikio ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA ambapo tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.

Asubuhi ya leo tutafakari HASIRA INAUMIZA ZAIDI YA TUKIO…
Kuna wakati watu wanaweza kufanya mambo yanayotuudhi sisi na hivyo kupelekea kupata hasira.
Lakini hasira hizi usipozidhibiti na kuzitatua, zinakuumiza zaidi kuliko hata lile tukio lililosababisha hasira hiyo.

Tukio la kukukasirisha linatokea mara moja tu, lakini hasira zinazotokana na tukio hilo utakaa nazo muda mrefu sana.
Utakuwa hujitendei haki kama utakubali kuendelea kuumizwa na hasira za tukio ambalo tayari lilishapita.
Kinachokuwa kinakuumiza wakati huo siyo tena yule aliyefanya kitu cha kukukasirisha, bali wewe mwenyewe.

Usikubali kuendelea kujiumiza kwa matukio ambayo tayari yameshapita. Tatua hasira zako, wasamehe waliokukosea na muhimu zaidi, jisamehe wewe mwenyewe.

Uwe na siku bora sana ya leo.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha