Kuna jina ambalo ulipewa na wazazi au walezi wako, hili lilikuwa jukumu lao kwako ulipokuwa mdogo na hukuweza kujichagulia jina mwenyewe.
Pia wapo ambao wamejipa au kubadili majina yao kwa sababu mbalimbali. Yote hayo ni majina ya kutumia kama utambulisho kwa wengine.
Lakini pia kuna jina jingine muhimu, hili ni lile jina ambalo wewe mwenyewe unalitengeneza. Siyo jina unalopewa na wazazi, wala kubadili mwenyewe. Bali ni jina ambalo watu wanakupa, kutokana na kile unachofanya.

Kutokana na unachofanya, na jinsi ambavyo unagusa maisha ya wengine, lipo jina ambalo unajitengenezea. Linaweza kuwa ni jina lako hilo hilo, lakini linapotajwa mbele ya watu, watu wanapata picha fulani ndani yao. Kwamba huyu ndiye yule mtu anayetusaidia kwenye eneo fulani, au huyu ndiyo yule mtu ambaye ni mzembe kwenye mambo mengi.
Kila kitu tunachokifanya kwenye maisha yetu, kinachangia katika kujenga jina letu. Watu wanatukumbuka na kututambua kupitia yale tunayofanya. Na kadiri jina lako linavyokuwa kubwa, ndivyo wengi zaidi wanavyojua kuhusu wewe na kutaka kunufaika na wewe pia. Au kukuepuka kama jina lako linatambulika kwa mabaya.
Watu kwa kujua kwamba jina ni muhimu, wamekuwa wakifanya jitihada za kutengeneza majina yao kwa njia zisizo sahihi. Wengi wamekuwa wakiigiza mambo ili wachukuliwe na watu kwa namna fulani. Wengine wamekuwa wakifanya vitu fulani ili tu kuvuta umaarufu kutoka kwa wengine.
SOMA; UKURASA WA 1012; Vitu Viwili Utakavyoenda Navyo Kaburini…
Unapojenga jina lako kwa mambo yasiyo asili, au mambo ambayo huwezi kuyaendeleza kwenye maisha yako, unajenga jina ambalo haliwezi kudumu, jina ambalo litaanguka haraka.
Jenga jina lako kwa yale mambo ambayo ni ya asili kwako, yale mambo ambayo uko vizuri sana. Kwa njia hii, jina utakalojenga litadumu na hata baada ya wewe kuondoka hapa duniani, utaacha jina hilo.
Jenga jina lako kwenye matendo, usiwe mtu wa kusema na kutaka kuonekana, bali kuwa mtu wa matendo na wa kusababisha. Hakikisha unazalisha kitu, unatoa matokeo yanayoweza kuwasaidia wengine na kufanya maisha yao kuwa bora zaidi.
Tatua jambo vizuri, fanya hivyo kila wakati na wawezeshe watu kuelewa kwa kina kiasi kwamba jina lako linaendana na tatizo au changamoto unayotatua.
Kadiri unavyoweka juhudi kwenye kujenga jina lako, kwa njia sahihi, ndivyo unavyoyaelekea mafanikio makubwa kwako.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog