Tunapenda kupiga hatua kwenye maisha, tunapenda kufanikiwa, lakini kinachotukwamisha mara nyingi ni njia tunazotumia kupiga hatua na kufikia yale mafanikio tunayotaka.
Kwa mfano, kuendelea kufanya kile ambacho mtu anafanya, kwa njia ambayo anafanya kutaendelea kuzalisha matokeo ambayo amekuwa anapata.
Haihitaji shahada kujua kwamba kama utaendelea kufanya kazi unayofanya, kwa namna unavyoifanya, utaendelea kupata matokeo unayopata sasa. Kadhalika kwenye biashara yako.
Hivyo hatua ya kwanza na ya muhimu kwenye mafanikio ni kubadilika. Kubadilika wewe na kuwawezesha wale wanaohusika na wewe kwa namna yoyote waweze kubadilika pia.

Lakini inapofikia kwenye kubadilika ndipo ugumu mkubwa unapoanzia, kwa asili watu hawapendi mabadiliko, kabisa yaani. Mabadiliko huwa ni magumu na mabadiliko huwa hayana uhakika, hivyo watu wanapenda kuendelea kufanya kile walichozoea kufanya.
Watu wanapojaribu mabadiliko na kuona ni magumu, haraka hurudi kufanya kile walichozoea kufanya. Na hakuna kitu ambacho watu watapingana nacho kama pale wanapogundua wengine wanawalazimisha kubadilika. Yaani kama unataka kuwabadili watu, unashindwa vibaya kwa sababu hakuna kitu watu hawapendi kama kubadilishwa.
SOMA; UKURASA WA 764; Samaki Huanza Kuozea Kichwani…
Hivyo basi, lazima zoezi hili la mabadiliko lifanywe kwa njia ambayo itakuwa bora, itakayokuwa na hamasa kwa wengi na pia itakayokuwa ya kudumu.
Na njia pekee ya kuweza kufanya mabadiliko makubwa na ya kudumu ni kutengeneza utamaduni. Utamaduni ni utaratibu wa maisha ambao mtu au watu wanaufuata. Hivyo unapoweza kutengeneza utamaduni, utaratibu wa maisha ambao unapelekea kupata yale matokeo ambayo unayataka, inasaidia zaidi.
Utaratibu unamfanya mtu au watu kuufuata kama njia ya maisha. Kwa mfano mtu anapofika kwenye eneo la huduma na kukuta watu wamepanga mstari, moja kwa moja na yeye atapanga mstari. Lakini akifika na kukuta watu wanagombania kupata huduma, na yeye atafanya hivyo.
Kwa kifupi watu wanafanya kile ambacho kimezoeleka kufanya. Na hata wewe mwenyewe unafanya kile ulichozoea kufanya. Hivyo ukitengeneza utaratibu mpya wa maisha yako na kwa wale wanaohusika na wewe, unatengeneza utamaduni mpya ambao watu watauishi.
Mwanzoni mwa kutengeneza utamaduni kutakuwa na changamoto na kupingwa au kujipinga mwenyewe, lakini kadiri muda unavyokwenda utaratibu unazoeleka na kuwa sehemu ya maisha.
Kazana kutengeneza utamaduni kwenye kila eneo la maisha yako, kuanzia maisha binafsi, kazi zako, biashara zako na hata kwenye familia.
Lakini pia kuwa macho, ukitengeneza utamaduni mbaya, utakuwa mgumu kwako kuuvunja.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog