“No man is free who is not master of himself” – Epictetus

Habari za asubuhi ya leo mwanamafanikio?
Hongera kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni nafasi bora na ya kipekee kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Msingi wetu wa maisha ya mafanikio ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA ambapo tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.

Asubuhi ya leo tutafakari UHURU NI KUWEZA KUJITAWALA…
Watu wengi tuna dhana isiyo sahihi kuhusu uhuru.
Wengi huwa tunafikiri kwamba uhuru ni kuweza kufanya chochote unachotaka, kwa wakati unaotaka bila ya kuzuiliwa na chochote.
Lakini huo siyo uhuru, kwa sababu kuna vitu ukishazoea kufanya, unakuwa mtumwa kwa vitu hivyo. Unakuwa huwezi tena kuacha kufanya, au huwezi kuwa na subira.
Na hapo unakuwa mtumwa wa matakwa yako mwenyewe.

Uhuru ni kuweza kujitawala wewe mwenyewe.
Kuweza kujiambia hapana kwa kitu ambacho unakitaka sana.
Uhuru ni pale unapoweza kupoteza chochote na bado maisha yakaendelea, usione kama umepoteza maisha yako kabisa.

Hata uwe na fedha nyingi kiasi gani, kama kuzipoteza kutakufanya ujute sana na kuona maisha hayafai, bado hujawa huru.
Hata kama una uwezo wa kupata chochote unachotaka, kama huwezi kujiambia hapana kwa muda fulani na kujinyima kile unachoweza kupata bado haupo huru.

Uhuru ni kuweza kujitawala, kuweza kutawala hisia na matakwa yako, kuweza kutawala tabia zako.
Na muhimu zaidi, kuwa tayari kupoteza chochote na maisha yako yakaendelea.

Je upo huru kiasi gani?
Tafakari hili leo na jijengee uhuru mkubwa zaidi kwenye maisha yako kwa kujitawala zaidi.

Ukawe na siku bora sana leo.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha