Make the best use of what is in your power, and take the rest as it happens. – Epictetus
Habari za asubuhi ya leo rafiki yangu?
Hongera kwa siku hii muhimu sana ya leo.
Hii ni siku mpya na ya kipekee sana kwetu ambapo tunakwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Msingi wetu wa maisha ya mafanikio ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA ambapo tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari NDANI YA UWEZO WAKO NA NJE YA UWEZO WAKO…
Kwenye maisha yako, kuna vitu ambavyo viko ndani ya uwezo wako, hivi ni vitu ambavyo kwa namna moja au nyingine unaweza kuviathiri, unaweza kuvibadili na kuvifanya utakavyo.
Lakini pia kuna vitu ambavyo vipo njebya uwezo wako, hivi ni vitu ambavyo huwezi kuviathiri kwa namna yoyote ile. Vipo kaka vilivyo na huwezi kuvibadili.
Ili maisha yako yawe bora, jua vile vitu ambavyo vipo ndani ya uwezo wako na weka juhudi kuvifanya kuwa bora kabisa. Vitumie vizuri, viboreshe zaidi na hakikisha unapata matokeo bora zaidi.
Na kwa vile vitu ambavyo havipo ndani ya uwezo wako, vipokee kama vinavyokuja, na angalia namna gani unaweza kwenda navyo kama vilivyo.
Kosa kubwa ambalo wengi wanafanya ni kushindwa kufanyia kazi vile vilivyo ndani ya uwezo wao, na kukazana kubadili vile ambavyo vipo nje ya uwezo wao. Hapa watu hupata matokeo mabovu kabisa ambayo hufanya maisha yao kuwa hovyo.
Jua vilivyo ndani ya uwezo wako na vitumie vizuri na vilivyo nje ya uwezo wako vipokee vizuri.
Uwe na siku bora sana ya leo.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha