Wapo watu ambao wamekwama, wakiamini kilichowakwamisha ni kukosa mawazo bora ya nini wafanye au hatua gani wachukue.
Lakini ukiangalia kwa undani, tatizo siyo wazo bora. Katika zama tunazoishi sasa, mawazo bora yapo mengi sana, mengi mno na yapo kila mahali.
Tunaweza kusema mawazo bora ni mengi kuliko uwezo wa mtu mmoja kuyafanyia kazi yote.
Tatizo kubwa mara zote limekuwa ni kuweza kufanya mambo yatokee, kuchukua hatua ambayo inazalisha matokeo bora.
Hili ndiyo tatizo kubwa ambalo linawazuia wengi kupiga hatua.

Na linakuwa tatizo kwa sababu;
Moja; kufikiri na kusema ni rahisi kuliko kufanya. Kufanya kunahusisha matumizi ya nguvu, ambayo wengi hawapendi kuyafanya.
Mbili; mwanzo ya jambo lolote ni mgumu, unapoanza kufanya chochote unakutana na vitu ambavyo hukutegemea kukutana navyo na hivyo mambo yanakuwa magumu.
SOMA; UKURASA WA 57; Dunia Haina Usawa…
Tatu; ipo hatari ya kushindwa, kwa chochote unachofanya, kuna nafasi ya kushindwa, na hii huwapa watu hofu ambayo inawazuia kuchukua hatua na kuona labda bado hawajawa tayari au hawajawa na wazo bora kabisa.
Nne; uvumilivu unahitajika sana kwenye kufanya, kwa sababu siyo kila unachofanya utapata matokeo unayotarajia kwa wakati unaotarajia. Utapata matokeo tofauti, utashindwa na hayo yote yatakuwezesha kuwa bora zaidi kama hutakata tamaa.
Tano; mazuri ya kufanya yapo mengi, hivyo mtu akikosa msimamo anajikuta anajaribu kila la kufanya. Kwa kujaribu jaribu huko mara nyingi kunamfanya ashindwe kupata matokeo bora.
Hivyo tatizo siyo wazo bora, tatizo ni kuweza kufanya mambo yatokee, kuweza kuzalisha matokeo bora kabisa.
Na utaweza hili kama utachagua kile unachotaka na kisha kukomaa nacho mpaka upate matokeo bora kabisa, usikubali kuyumbishwa na chochote.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog