The greatest remedy for anger is delay. – Lucius Annaeus Seneca
Hongera rafiki yangu kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Siku hii bora na ya kipekee kabisa kwetu, tunakwenda kuweka juhudi kubwa ili tuweze kupata matokeo bora sana.
Msingi wetu wa maisha ya mafanikio ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA ambapo tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari TIBA YA UHAKIKA YA HASIRA…
Tiba ya uhakika ya hasira ni subira,
Pale unapopata hasira kutokana na jambo lolote lile, usikubali kusukumwa na hasira zako kusema au kufanya lolote.
Badala yake subiri, kaa kimya na vuta pumzi.
Jipe muda wa kusubiri mpaka pale unapohakikisha kwamba akili yako imekaa vizuri.
Unapokuwa na hasira, unakuwa unaendeshwa na hisia na siyo fikra.
Hivyo jambo lolote unalofanya ukiwa na hasira huwa halitokani na fikra zako sahihi, badala yake linatokana na hisia unazokuwa nazo kwa wakati huo.
Ndiyo maana mengi unayosema au kufanya ukiwa na hasira, unaishia kuyajutia pale hasira zinapoisha.
Hivyo ukitumia tiba hii ya hasira, tiba ya kuwa na subira, unaruhusu hisia zishuke na akili zako zirudi.
Hata kama umepatwa na hasira kiasi gani, jipe dakika chache za kusubiri, jipe dakika chache za kupumua na utajiepusha na matatizo makubwa zaidi.
Ukawe na siku bora sana leo rafiki yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha