Tuongee jambo moja muhimu sana, ambalo naona wengi tunalisahau hasa kwenye zama hizi za utitiri wa fursa ambazo zinaonekana kuwawezesha watu kupata fedha.

Kuna kupata fedha mara moja, au mara chache na kuna kupata fedha kwa muda mrefu. Yaani haya mawili ni sawa na mtu unakinga maji kwa mvua inayonyesha mara moja moja na mwingine ambaye ana chemchem inayotiririsha maji wakati wote.

Ni rahisi kupata fedha mara moja au mara chache, unaweza kuwadanganya au kuwahadaa watu na ukapata fedha. Unaweza kukutana na fursa isiyo ya kweli, lakini kwa kuwa watu hawajaijua kiundani wakaingia na ukapata fedha.

wp-image--1475273682

Lakini kupata fedha za kila mara na kwa kipindi kirefu, labda maisha yako yote ni kitu kigumu. Ni kitu ambacho kinakutaka ujenge misingi imara ya kukuwezesha kutengeneza kipato kisichokauka.

Inakuhitaji uwe na maono makubwa, na maono ambayo yanawawezesha wengine kuwa na maisha bora sana. Maono ambayo wewe utayaishi kila siku ya maisha yako, utapambana nayo na kuhakikisha umetengeneza mfumo ambao fedha zitaingia kila wakati.

SOMA; UKURASA WA 991; Kinachoota Haraka, Hupotea Haraka…

Kumbuka hili kila wakati unapokutana na fursa au unaposhawishiwa kwamba kitu fulani ni fursa na watu wanapata fedha. Jiulize je wanapata fedha mara moja au mara chache au upo uwezekano wa kuendelea kupata fedha kila wakati? Na je ni kitu ambacho unaweza kuendelea kukifanya kila wakati kwenye maisha yako yote?

Fedha ni zao la kuwa na maono makubwa, na haijalishi kwamba unapata faida kubwa kwa wakati mmoja, bali kukomaa na maono yako, kwa muda mrefu kutakutengenezea mfereji wa kukuingizia fedha mara zote.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog