First say to yourself what you would be; and then do what you have to do. – Epictetus
Habari za asubuhi ya leo mwanamafanikio?
Siku hii nzuri sana na ya kipekee kwetu ni nafasi bora ya kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora.
Msingi wetu wa maisha ya mafanikio ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA ambapo tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari JIAMBIE KISHA FANYA…
Ili kupata kile unachotaka kwenye maisha yako, ili kupiga hatua na kufanikiwa, unahitaji kufanya mambo mawili muhimu.
Jambo la kwanza jiambie unataka kuwaje, jiambie unataka kufika wapi, jiambie nini unataka kwenye maisha yako.
Ni muhimu sana ujiambie kwa sababu kwa kujiambie unaifanya akili yako kutengeneza mazingira ya kupata kile unachotaka. Unajiweka kwenye nafasi ya kuzikwepa kelele mbalimbali na kukazana na kile ambacho unakitaka hasa.
Jambo la pili fanya kile unachopaswa kufanya ili kufika unakotaka kufika.
Kujiambia ni hatua ya kwanza na ndogo, ili kupata kile hasa unachotaka, unahitaji kuchukua hatua na kufanya.
Unahitaji kuweka juhudi kwenye kile ulichojiambia. Hata ujiambie kwa msisitizo kiasi gani, kama hufanyi ni kazi bure.
Asubuhi hii tafakari ni mambo gani umekuwa unajiambia na hatua gani ambazo umekuwa unachukua ili kufikia yale unayojiambia.
Uwe na siku bora sana ya leo.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha