Watu wengi wanapochagua kazi au biashara ya kufanya, huanza kuangalia ni kiasi gani cha fedha wanaweza kupata. Na kama kuna machaguo mengi ya vitu wanaweza kufanya, wengi huchagua kile wanachoona kitawalipa zaidi.
Wapo wengine wanasema wazi kabisa kwamba wapo tayari kufanya chochote kama kinawaingizia fedha.
Hali kama hii ni kawaida pale mtu anapoanzia chini, pale ambapo mtu hana fedha na maisha ni magumu, lazima maamuzi yasukumwe na fedha. Ni sawa na mtu ambaye amekosa hewa, chochote utakachomwambia hakitamsaidia, muhimu zaidi kwake ni kupumua.
Changamoto huja baada ya watu kupata hizo fedha wanazokuwa wanazitafuta, wanakuwa wameshaondoka kwenye ile hali kwamba fedha hakuna. Na hapo sasa ndipo wanapoanza kuona uhalisia wa lile chaguo walilofanya. Hapo ndipo wanaanza kuona kile walichochagua kufanya hakiwaridhishi, au hakitoki ndani ya mioyo yao kweli.

Hapa ndipo wengi hujikuta wameingia kwenye gereza ambalo wamejitengenezea wao wenyewe. Pale wanapogundua maisha wanayotengeneza kupitia kazi au biashara wanayofanya, siyo aina ya maisha waliyokuwa wanayataka, au maisha wanayoweza kujivunia nayo.
SOMA; BIASHARA LEO; Wateja Wako Wanatamani Sana Kitu Hichi Kimoja Kutoka Kwako…
Hivyo rafiki, unapofanya maamuzi yoyote kwenye kazi au biashara, japo unaweza kuwa na uhitaji mkubwa wa fedha, usiangalie fedha pekee, angalia pia aina ya maisha unayotengeneza kupitia kazi au biashara hiyo. Jione ndani ya kazi au biashara hiyo kwa miaka yako yote. Je ni kitu kinachokupa kuridhika na kuona maisha yako yana maana?
Kama huyafurahii na kuyapenda maisha yako unayotengeneza kupitia kile unachofanya, unajitengenezea mtego ambao utakuumiza baadaye. Na kama unachoangalia ni fedha, ni vyema ukakumbuka kwamba, chochote unachochagua kufanya kinaweza kukuingizia kipato kama utakuwa tayari kuwasaidia wengine na kuwa mvumilivu.
Angalia aina ya maisha unayojitengenezea kupitia kile unachotaka kufanya, kabla hata hujaangalia kiasi cha fedha unachopata. Kuna kiwango cha fedha ukishafikisha, hutakumbuka tena kuhusu fedha bai aina ya maisha unayoishi. Na hilo litakutesa kwa maisha yako yote.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog