The key is to keep company only with people who uplift you, whose presence calls forth your best. – Epictetus

Habari za asubuhi ya leo mwanamafanikio?
Hongera kwa siku ya leo, nafasi nyingine nzuri na ya kipekee kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa.
Kama kuna chochote ambacho jana ulisema utafanya kesho, basi nakukumbusha kesho yenyewe ndiyo leo.
Msingi wetu wa maisha ya mafanikio ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA ambapo tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.

Asubuhi ya leo tutafakari ZUNGUKWA NA WANAOKUVUTA KWENDA JUU…
Wale wanaotuzunguka wana mchango mkubwa sana wa pale tulipo sasa.
Kama unazungukwa na watu ambao wanaweka juhudi na wanataka wengine waweke juhudi, wewe pia utaweka juhudi na kupiga hatua.
Kama unazungukwa na watu ambao wamekata tamaa na hawana kubwa wanalofanya, wewe pia utakata tamaa.

Ukizungukwa na watu ambao wana kitu cha kukosoa kwenye kila jambo, wana kila sababu kwa nini jambo haliwezekani, hata uwe na hamasa kiasi gani, utaishia kukata tamaa na kuona haiwezekani.
Lakini ukizungukwa na watu wanaokusukuma kuchukua hatua, wanaokupa sababua ya kufanya, hamasa yako itakuwa kubwa na kuweza kuchukua hatua.

Leo wamulike wale wote wanaokuzunguka na angalia kama wanakusukuma kwenda juu au wanakuvuta kwenda chini. Angalia kama ukiwa nao unapata hamasa ya kuchukua hatua au unakata tamaa na kuona mambo hayawezekani.

Kama umezungukwa na wanaokukatisha tamaa na kukurudisha nyuma, salama yako ni kukaa mbali na watu hao. Kwa sababu hawatakuruhusu upige hatua kabisa.
Kumbuka watu walioshindwa wanapenda kuzungukwa na watu walioshindwa. Hivyo kuwa makini sana.

Ukawe na siku bora sana ya leo.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha