Tabia ya binadamu ni moja, ukiwa kwenye kazi fulani, unaona kama kazi hiyo haina fursa na kazi za wengine ndiyo zina fursa zaidi na manufaa zaidi. Kadhalika kwenye biashara, mtu anaweza kuwa kwenye biashara fulani, lakini akiwaangalia wengine ambao wapo kwenye biashara nyingine, anaona wana manufaa zaidi kuliko yeye.

Lakini ukweli ni kwamba, bado zipo fursa nyingi sana kwenye kazi au biashara yoyote anayofanya mtu kabla hajaanza kuangalia kwingine. Ninachomaanisha ni kwamba, hapo ulipo wewe, bado zipo fursa nyingi, bado kuna nafasi ya kupiga hatua zaidi kabla hujaanza kuangalia kwingine.

Maisha Hayajawahi

Na fursa hizi zipo kwa sababu wengi wanafanya kwa viwango vya kawaida sana. Wengi wanafanya kazi ili tu kuonekana wanafanya kazi, wanafanya kama ambavyo wengine wanafanya na hakuna juhudi za ziada wanazoweka. Hata kwenye biashara pia, wengi wanafanya kama wengine wanavyofanya, wanafanya kupata fedha ya kusukuma maisha na zaidi ya hapo hakuna kingine.

SOMA; Nyasi Za Upande Wa Pili Ni Za Kijani Zaidi…

Hivyo pale ulipo sasa, iwe unafanya kazi au biashara, ukiamua kuweka juhudi kubwa, ukiamua kwenda hatua ya ziada, ukiamua kufanya zaidi ya wengine wanavyofanya, kwa hakika utapata zaidi ya unavyopata sasa.

Kama utaamua kutoa thamani kubwa kwa wengine, kama utaamua kwenda mbele zaidi, kuacha mazoea na kuongeza ubunifu kila siku, utagusa mgodi ambao wengi huwa hawaufikii.

Fursa zaidi zipo kwa wale ambao wapo tayari kuweka kazi ya ziada, waliopo tayari kubadili kwa kiasi kikubwa na kuweka ubunifu unaoongeza thamani kwa wengine.

Upo usemi kwamba nyasi za upande wa pili huwa zinaonekana ni za kijani zaidi ya nyasi zilizopo upande wetu. Lakini kabla hujakimbilia nyasi hizo unazoona ni za kijani zaidi, jiulize je umekazana kuzifanya nyasi zako kuwa za kijani zaidi?

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog