Miaka michache iliyopita nilipokuwa safarini kuelekea mkoa wa Mbeya kwenye semina ya kitaaluma lilinijia wazo hili la kuanza kushauri marafiki, ndugu na jamaa mbalimbali kuhusu umuhimu wa kuwa na makazi bora. Ni wazo ambalo lilikuja kwenye kichwa baada ya kuona na kutafakari kwa kina maisha na mazingira duni wanayoishi baadhi ya watu kwenye jamii zetu. Ni mazingira ambayo wengi wetu tumezaliwa na kuishi kwa miaka kadhaa kiasi kwamba tukaamini kuwa ni kawaida na tunapaswa kuwa na makazi duni kiasi hicho. Wanaoishi kwenye makazi duni ni wazazi wetu, kaka zetu, dada zetu na wadogo zetu ambao kwa namna tofauti wapo hatarini dhidi ya athari hasi zitokanazo na kuwa na mazingira hatarishi dhidi ya binadamu. Kile nilichofundishwa darasani kwa miaka mingi sicho nilichokiona kwenye mazingira yetu halisi bali ni kinyume chake, hakika ni safari ambayo ilibadili mtazamo wangu wa maisha ya kitaaluma.

Leo hii bado naendelea kuhamasisha watu waweze kuwa na nyumba bora ambazo ni haki yetu wote bila kuweka sababu zozote zile ambazo zimesababisha kuwepo na utofauti wa maendeleo ya kiuchumi na kijamii. Furaha ya nafsi yangu ni kuona tunapiga hatua kubwa kwa kila mmoja wetu kuanza kuishi kwenye nyumba bora kwa matumizi yoyote ambayo umelenga kuitumia. Ukweli ni kwamba hii sio safari rahisi lakini inawezekana endapo tutakuwa na dhamira ya dhati katika kutimiza malengo yetu.

majengo 41

Yamkini na wewe pia umedhamiria kuanza au kuendelea na ujenzi ambao kwa namna moja au nyingine utakuwa unatimiza malengo yako kwa kile ambacho unakwenda kukijenga. Ombi langu kwako ni kuhakikisha kuwa unajenga kwa ufanisi mkubwa ili iwe chachu kwa maendeleo yako binafsi na kwa jamii inayokuzunguka. Leo hii napenda kukupa baadhi ya fursa ambazo unapaswa kuzitazama kwa namna ya tofauti pale unapotaka kuwekeza kwenye majengo.

MAJENGO YA MAKAZI NA BIASHARA

Mara nyingi wazo lako la kwanza la kutaka kuanza ujenzi kwenye maisha yako utaanza kufikiria kuhusu nyumba za makazi na biashara. Nyumba za makazi hujengwa kwa matumizi mbalimbali ya kibinadamu ikiwamo malazi, ni nyumba ambazo zitamfanya mtumiaji kuwa katika hali ya hamasa na utulivu wa mwili na akili. Nyumba za biashara hujengwa kwa matumizi yoyote ya kibiashara ambayo yataendana na lengo la mtumiaji dhidi ya mazingira. Hapa nazungumzia majengo mbalimbali kwa matumizi ya maduka, ofisi, vituo vya mafuta, migahawa, hoteli, soko na saluni za kisasa. Ni muhimu sana ukawa na dira ya matumizi halisi ya nyumba unayotaka kuijenga dhidi ya uwezo halisi wa kipato chako ili kuepuka kutumia miaka mingi kwenye ujenzi na kupunguza uwezekano wa kushindwa kukamilisha ujenzi kutokana na sababu mbalimbali zinazoweza kujitokeza.

SOMA; MAMBO MUHIMU YA KUZINGATIA KUIFANYA NYUMBA YAKO KUWA BORA NA SALAMA

MAJENGO YA VIWANDA NA MAGHALA

Majengo ya viwanda ni nyumba ambazo hujengwa kwa matumizi ya uzalishaji wa bidhaa mbalimbali kwa matumizi yoyote yanayohitajika kwenye jamii. Ni majengo ambayo hubuniwa na kusanifiwa kulingana na aina ya kiwanda kinachokwenda kujengwa. Majengo ya maghala ni nyumba ambazo hujengwa kwa matumizi ya kuhifadhi vitu au bidhaa mbalimbali kwa sababu mbalimbali za kiuchumi ikiwemo kuhifadhia malighafi zinazopaswa kutumika kiwandani au kuhifadhia bidhaa mbalimbali zinazopaswa kuingia kwenye soko. Mara nyingi majengo haya hujengwa na watu wenye nia ya kuwa wawekezaji kwenye kampuni za uzalishaji au kuwa wakala wa bidhaa au malighafi kwenye taasisi au kampuni. Anza leo kutimiza malengo yako na kuwa sehemu ya mafanikio ya kiuchumi kwenye jamii yako. Tumia macho na akili kubwa ya kutathmini fursa mbalimbali zilizopo kwenye jamii yako na anza kuifanyia kazi kwa usahihi hata kwa hatua chache unazoweza kwa sasa mengine utaendelea kuyaweka sawa kadri yatakavyojitokeza.

MAJENGO YA STAREHE NA BURUDANI

Majengo ya starehe na burudani ni nyumba ambazo hujengwa kwa matumizi ya kuwafanya watu kuwa na hisia za furaha na amani. Ni majengo ambayo hubuniwa na kusanifiwa kwa namna ambayo itakidhi vigezo vya matumizi na idadi ya watumiaji husika kwa wakati mmoja. Majengo haya hujengwa kwa matumizi mbalimbali ya starehe na burudani yakiwemo matamasha ya muziki, maigizo, mikutano, baa, kasino, kumbi za sherehe, semina, viwanja mbalimbali vya michezo na klabu za muziki. Jamii nzuri na bora lazima ipate muda wa kupumzisha na kuburudisha mwili na akili ili kuweka mwili katika hali ya msawazo ili kuwa wezesha kuwa wazalishaji bora kwenye shughuli zao za kiuchumi na kijamii. Majengo haya huzingatia sana tamaduni za jamii husika na mabadiliko halisi ya ukuaji wa sekta mbalimbali za sanaa na michezo ikiwemo sekta ya muziki, maigizo, mpira wa miguu, mpira wa kikapu na burudani mbalimbali. Bado tuna uhaba mkubwa sana wa sehemu nzuri na sahihi za burudani za kisasa, iwezeshe jamii yako ipate sehemu nzuri ya kupumzika na kufurahia maisha baada ya shughuli mbalimbali za kiuchumi na kijamii.

MAJENGO YA HUDUMA ZA AFYA NA ELIMU

Majengo ya huduma za afya ni nyumba ambazo hujengwa kwa matumizi na viwango tofauti katika utoaji wa huduma za afya kwa viumbe vyote ikiwemo binadamu na wanyama wengine. Majengo haya hujumuisha zahanati, vituo vya afya, hospitali, maabara na vituo vya mazoezi ya viungo katika kuboresha afya za viumbe hai. Majengo ya elimu ni nyumba maalumu ambazo hujengwa kwa matumizi ya utoaji wa elimu kwa jamii. Majengo ya shule za awali, shule za msingi, shule za sekondari, vyuo vya kati na vyuo vikuu huwa na utofauti kutokana na vigezo mbalimbali ambavyo huwekwa ili yaweze kukidhi matakwa maalumu ya matumizi husika. Epuka ubadilishaji holela wa nyumba za matumizi ya makazi na kuzitumia kwa matumizi ya utoaji huduma za afya na elimu. Tunahitaji majengo na miundombinu ya kisasa ambayo itatuwezesha kupiga hatua kubwa ya kielimu na kuboresha afya ya jamii. Jamii yetu bado inakuhitaji sana wewe ili uweze kuwekeza kwenye aina hii ya majengo kwa kuwa bado tuna uhaba mkubwa sana kwenye miundombinu ya utoaji wa huduma hizi.

SOMA; Zifahamu Hatua Muhimu Za Uwekezaji Wa Ardhi Na Majengo, Je Upo Hatua Gani Kuelekea Mafanikio Yako?

MAJENGO YA UFUGAJI NA KILIMO

Majengo ya ufugaji na kilimo ni nyumba na miundombinu mbalimbali ambayo hujengwa kwa matumizi ya kuwa wezesha wakulima na wafugaji waweze kufanya shughuli zao kwa ufanisi na ubora pasipo kuathiri mazingira na watumiaji wengine wa ardhi. Majengo haya hujumuisha nyumba za malazi na malisho ya mifugo, vitalu, nyumba za uchinjaji wa mifugo, nyumba za kuoshea mifugo na mazao. Haya ni majengo ya kisasa ambayo ni rafiki wa mazingira na kuepusha migogoro dhidi ya watumiaji wengine kwenye eneo husika. Mabadiliko yoyote yanayotokea kwenye jamii yetu yanatokana na msukumo mkubwa wa mabadiliko ya kiuchumi, kisiasa na kijamii. Ongezeko kubwa la uhitaji wa ardhi kwa kiasi kikubwa umesababisha mabadiliko makubwa ya mbinu mbalimbali za uzalishaji na uendeshaji wa kilimo na ufugaji. Hivyo ni muhimu sana ukatafakari kuhusu namna bora ya utendaji na utunzaji wa shughuli zako za kilimo na ufugaji kwa kuwa siku za usoni kutakuwa na sheria kali sana zitakazo ratibu utunzaji wa mazingira na matumizi bora ya ardhi.

Tafakari yako kuhusu Makala hizi ni muhimu sana…..!!!! maoni na maswali yako ni mambo ambayo nayazingatia sana. Usisite kuwasiliana nami endapo dhamira yako itakusukuma kufanya hivyo. Karibu sana.

Tuendelee kuwa pamoja kupitia AMKA MTANZANIA tufike kwenye kilele cha mafanikio, pia endelea kufuatilia makala zijazo ili ujifunze zaidi.

Mwandishi wa makala hii ni mwanataaluma wa ujenzi.

Anapatikana kwa: Simu: +255 685 729 888

Baruapepe: kimbenickas@yahoo.com