Tunaishi kwenye dunia ambayo kila kitu kinapimwa kwa namba. Kuanzia fedha, kiwango cha kazi tunachofanya na hata idadi ya watu tunaowahudumia au kuwauzia.
Kipimo kikubwa sasa kimekuwa ni namba, na kadiri namba inavyokuwa kubwa, ndivyo tunavyoona tumefanikiwa. Kadiri kiasi cha fedha kinavyokuwa kikubwa, ndivyo tunavyoona tumefanikiwa. Kadiri idadi ya watu tunaowahudumia inavyokuwa kubwa, ndivyo tunavyoona tumepiga hatua.
Hakuna ubaya wowote kwenye namba, kwa sababu ni njia nzuri ya kupima tunaelekea wapi. Lakini pale namba zinapokuwa ndiyo kitu pekee ambacho tunaangalia, shida inakuwa kubwa.

Tunapoanza kuwaangalia watu kama namba, kwa idadi tunayowahudumia au kwa kiasi wanacholipia, tunasahau utu wao na kukazana na namba zetu. Na hapo ndipo tunapowapoteza watu hao, kwa sababu wanakosa ule utu kutoka kwetu pale tunapokazana na namba.
Ni muhimu sana watu unaokutana nao kwenye kazi au biashara zako, uwatendee kama watu, ambao wana matatizo na changamoto zao, ambazo wanahitaji suluhisho. Kwa njia hii utawafanya wajisikie wa thamani wanapojihusisha na wewe na hivyo kuendelea kuwa na wewe zaidi.
SOMA; UKURASA WA 972; Pamoja Na Changamoto Zao, Maisha Yetu Hayana Maana Bila Ya Watu…
Usikazane na namba pekee, kwa sababu zitakuzuia kuona kile muhimu, ambacho ni kwa namna gani umeyafanya maisha ya mtu kuwa bora zaidi. Ni kwa namna gani unachofanya kimeweza kuleta matokeo bora kwa wengine.
Namba ni nzuri kwa kipimo, lakini siyo nzuri katika kujenga mahusiano bora. Na kazi na biashara za sasa, zinahitaji zaidi mahusiano bora baina ya watu na siyo tu mategemeo ya kile mtu anaweza kupata.
Hudumia watu wenye matatizo na changamoto ambazo unawawezesha kuzitatua, usikazane na namba pekee.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog