Habari za leo rafiki yangu?

Hongera kwa siku hii nyingine nzuri kwetu, siku ambayo tuna nafasi ya kufanya makubwa na kupiga hatua zaidi. Haijalishi jana ilikuwaje, na wala haijalishi kesho tunapanga lini, muda tulionao leo ni muda unaotutosha kufanya yale ambayo yatafanya maisha yetu kuwa bora zaidi.

Kila zama zina kitabu chake, ndivyo wanavyosema Waswahili. Na mimi nakubaliana nao, lakini nina ya kuongeza kidogo, kwenye vitabu hivi vya kila zama, havitofautiani sana, kikubwa kinachobadilika ni changamoto na fursa.

Misingi ya mafanikio kwenye kila zama ni ile ile, mbinu za mafanikio ni zile zile, lakini fursa za mafanikio zinabadilika kila zama na hata changamoto zinabadilika kila zama.

Wakati wa zama za mawe, fursa za mafanikio ilikuwa kuokota matunda na kuwinda, vitu ambavyo mawe yaliweza kusaidia. Zikaja zama za chuma ambapo kilimo kilishika kazi pamoja na shughuli nyingine ambazo ziliweza kufanyika kwa vifaa vya chuma.

Zilipokuja zama za mapinduzi ya viwanda, mambo yalibadilika kabisa, yaani ilikuwa ni kama dunia inafahamika upya. Hapa fursa ziliongezeka na kuwa nyingi, pamoja na nafasi za ajira na hata biashara kupitia bidhaa zinazozalishwa viwandani. Lakini changamoto pia zikawa kubwa kuanzia ugumu wa kazi na kukosekana kwa uhuru kwenye kazi hizo.

Sasa tupo kwenye zama za taarifa, zama ambazo kwa siku moja mtu unapata taarifa na maarifa mengi kuliko ambavyo mtu angeweza kupata kwa miaka kumi karne ya 15. Mtoto wa miaka kumi zama hizi ana maarifa na taarifa ambazo mfalme hakuweza kuwa nazo kwenye karne ya 15. Ni mabadiliko makubwa ambayo kadiri siku zinavyokwenda, ndivyo yanavyozidi kuwa makubwa zaidi.

NUFAIKA NA MABADILIKO

Lakini zama hizi pia zina changamoto zake, na changamoto kubwa kabisa ni mbili; moja wingi wa fursa na hivyo watu kutangatanga na fursa na kujikuta wanakosa kabisa, hii imeanza kuitwa kufa kwa ku ya fursa huku umezama kwenye bahari ya fursa. Mbili ni kasi ya mambo yanavyokwenda, mambo yanakwenda kasi sana kiasi kwamba watu hawaelewi nini kinaendelea. Wengi wanaachwa nyuma kwa kushindwa kwenda na kasi. Na wapo wanaoenda nayo lakini pia inawapoteza.

Kwenye makala hii ya leo, nakwenda kukushirikisha kitu kimoja muhimu ambacho ukiwa nacho, kitakuwezesha kukabiliana na changamoto hizo mbili ili kuweza kwenda sawa na zama hizi. Itakuwezesha kuchagua fursa sahihi kwako na kuifanyia kazi mpaka kuona matunda mazuri ya fursa hiyo. Pia itakuwezesha kwenda sawa na kasi inayoendelea kwenye dunia ya sasa.

Wingi wa fursa umewafanya watu kuchanganyikiwa kabisa, kwa sababu mtu anakutana na fursa moja, anaona inamfaa, anaanza kuifanyia kazi, wakati anaendelea, anaona fursa nyingine ambayo inaonekana ni nzuri kuliko ile ya awali. Anaacha ile na kwenda kwenye hiyo mpya, akiwa anaanza anaona nyingine nzuri zaidi. Hapa ndipo mtu anajikuta akihama hama kwenye kila aina ya fursa, na mwisho wa siku hakuna anachokuwa amekamilisha.

Kutokana na kasi kubwa ya mambo yanavyoenda sasa, watu wanataka vitu na wanavitaka sasa. Ile hali ya kusubiri kitu kitokee inatoweka kabisa. watu wanaona kama wanachelewa hivyo kitu kikichukua muda wanaachana nacho nakutafuta kingine ambacho wanaweza kufanya au kupata kwa haraka. Hali hii ya kasi imewafanya wengi kukimbizana na vitu vingi na mwisho wa siku wasione wamekamilisha nini.

Kitu pekee cha kukuwezesha kuepuka changamoto hizi kubwa za zama tunazoishi ni KUWA NA SUBIRA. Ni kitu rahisi kusema na huenda utasema najua hilo, lakini ni kitu kigumu mno katika utekelezaji. Na ndiyo maana leo nataka nikueleze vizuri rafiki yangu ili uwe na hatua sahihi za kuchukua.

Unapokuwa na subira kwenye maisha yako na mambo yako, inakupa wewe utulivu wa kuweza kufanyia kazi yale ambayo ni ya muhimu kabisa kwako. Subira inakuwezesha kuchagua kipi hasa unachotaka, kisha kukifanyia kazi hicho na kuacha na mengine yote. Subira inakusaidia kuondoka kwenye hali ya kasi, ya kutaka kitu na kukitaka sasa, kujua kila kitu kinahitaji muda na hivyo kuhakikisha unatoa muda huo.

Subira ni kitu kigumu kukiishi kwa sababu ya jinsi dunia inavyoenda. Sisi binadamu ni viumbe wa kijamii, huwa tunafanya yale ambayo wengine wanafanya. Kwa kifupi tunahamasishwa na wengine, hivyo inapokuja kwenye mambo kama fursa mpya, ni vigumu sana wewe kuacha fursa ambayo kila mtu anaifanyia kazi na kuisifia. Hivyo wengi wamekuwa wakibebwa na kundi kama hivyo na kujikuta wakihangaika na kila aina ya fursa. Pia subira ni ngumu pale unapokuwa umeshajizoesha kupata kile unachotaka kwa wakati unaotaka wewe. ukiambiwa usubiri unaona kama kuna kitu kikubwa unapoteza.

Subira inahitaji ukomavu wa kifikra na kiimani, subira inahitaji uzoefu wa kufanya na kukosea, ndiyo maana wengi hawana subira. Lakini ukianza sasa kufanyia kazi kujijengea subira, utaweza kuwa nayo na itakusaidia sana.

Unachohitaji katika kujenga subira ni kitu kikuu kimoja, kujua hasa ni nini unataka, kisha kufanya maamuzi ya kufanya kile pekee. Kukataa kubebwa na kila aina ya upepo unaojitokeza na kuwabeba wengine.

Pia jua kwamba, mwisho wa siku kila fursa ina faida kama mtu ataweka kazi kweli, na hivyo kuacha tamaa ya kuona kuna sehemu ni rahisi zaidi ya nyingine.

Mwisho kabisa, ni muhimu kukumbuka kwamba dunia inafanya mambo yake kwa namna yake yenyewe. Na wala haifanyi kama wewe unavyotaka. Hivyo unaweza kupanga vitu unavyotaka na usivipate, dunia ikakupa vitu vingine kabisa. unahitaji subira ili kuweza kuweka juhudi kupata kile hasa ambacho mtu unakitaka.

Subira ni silaha muhimu sana kwenye zama tunazoishi sasa, kama huna subira, ni vigumu mno kufanikiwa. Kwa sababu nguvu na muda ulionao vina ukomo, ila maarifa na fursa ni kama hazina ukomo zama hizi. Usipojijengea subira, utakimbizana na kila kitu mpaka siku unaondoka hapa duniani, na mbaya zaidi utaondoka hujakamilisha lolote kubwa.

Nakukumbusha semina yetu ya kuanza mwaka 2018, kama bado hujajiunga kushiriki semina hii bonyeza maandishi haya kupata maelezo ya semina hii.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA www.kisimachamaarifa.co.tz/kujiandikisha

Kupata huduma za Ukocha; www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha

Kujiunga na Kundi la kusoma vitabu; www.amkamtanzania.com/kurasa

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog