May be is very well, but Must is the master. It is my duty to show justice without recompense. – Lucius Annaeus Seneca
Asubuhi njema kwako rafiki yangu.
Hongera kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo, siku ambayo tumepata nafasi bora na ya kipekee kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Msingi wetu wa maisha ya mafanikio ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA ambapo tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari JIJUE KISHA JITUMIE KWA USAHIHI…
Unapokwenda kununua kitu chochote cha kutumia, huwa unapewa kitabu cha maelekezo.
Unaambiwa mambo ya kufanya na kutokufanya na kifaa hicho unachonunua.
Pia utapewa maelekezo ya hatua za kuchukua pale kifaa kinapoleta matatizo.
Lakini wewe umepokea akili na mwili wako, vitu vyenye nguvu kubwa sana kwenye maisha yako, ila hukupewa kitabu cha maelekezo ya jinsi ya kutumia.
Hilo ni jukumu ambalo wewe mwenyewe unapaswa kulifanya, na kadiri unavyolifanya mapema na kwa usahihi, ndivyo unavyonufaika.
Ili uweze kupiga hatua kubwa kwenye maisha, ili uweze kufika pale unapotaka kufika, lazima ujijue wewe mwenyewe kwanza.
Changamoto ni kwamba hakuna atakayekusaidia hilo,
Na halitakuwa zoezi rahisi,
Litakuwa zoezi la kujaribu na kushindwa,
Litakuwa zoezi linalokuhitaji upate muda wa kukaa na kujichunguza kwa kina.
Lakini ni zoezi litakalokulipa sana.
Usikubali kuendelea na maisha yako kama bado hujajijua wewe mwenyewe.
Jijue, kisha jitumie kisawasawa,
Ilo unapoondoka hapa duniani, basi uwe umeacha alama fulani.
Ukawe na siku bora sana ya leo.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha