Ukweli ni kwamba, mafanikio ni magumu, kuyatafuta mafanikio ni safari ngumu ambayo imejaa vikwazo na kukatishwa tamaa kwenye mambo mengi. Lakini hata unapoyapata mafanikio, siyo kwamba mambo yanakuwa rahisi, badala yake yanazidi kuwa magumu zaidi. Changamoto ndiyo zinazidi kuwa kubwa, na hatari ya kupoteza chochote ulichonacho inazidi kuwa kubwa.
Kwa kuangalia hilo kwa kina, mtu anaweza kujiridhisha kwamba haina maana kuhangaika na mafanikio, kwa sababu ni kukaribisha matatizo zaidi. Lakini hata tukiangalia kutokuwa na mafanikio, tukiuangalia umasikini, nao ni mgumu zaidi. Kuishi maisha yasiyo na mafanikio ni kugumu, matatizo ni mengi na kukosa uhuru ni kukubwa na kuna wakati utakwama usijue kipi cha kufanya.

Hivyo rafiki, lazima ukubali kwamba hakuna ambacho kitakuwa rahisi, hakuna. Iwe utachagua njia ya mafanikio, utakutana na magumu yake. Na hata ukichagua njia ya kutokuwa na mafanikio, utakutana na magumu yake.
SOMA; UKURASA WA 783; Ubinafsi Muhimu Kwako…
Ukichagua njia ya mafanikio utakosa usingizi kwa sababu ya changamoto unazoweza kuwa unakutana nazo kwenye mafanikio yako. Na hata ukichagua njia ya umasikini utakosa usingizi ukifikiria maisha ya kesho yanakwendaje, au gharama za maisha utalipaje.
Mafanikio na umasikini vyote vina gharama kubwa za kulipa, vyote vinahitaji kazi kubwa ya kufanya. Hivyo ni vyema ukachagua mafanikio, ni bora ukaweka juhudi kwenye kupiga hatua zaidi kuliko kubaki kwenye umasikini.
Hakuna chochote utakachofanya kwenye maisha ambacho kitakuondolea matatizo yote kabisa, labda siku utakapokufa. Lakini kama upo hai, matatizo na changamoto ni sehemu ya maisha yako. Jitoe kufanikiwa na jiandae kupambana na matatizo utakayokutana nayo kwenye safari yako.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog