Habari za leo rafiki yangu?

Hongera kwa nafasi hii nzuri sana ya leo, ni nafasi ya kipekee kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa katika kuelekea kwenye mafanikio yetu.

Safari yetu ya mafanikio haijanyooka, zipo changamoto na vikwazo vingi ambavyo vimekuwa vinawazuia wengi kufanikiwa.

Katika makala hizi za USHAURI WA CHANGAMOTO nimekuwa nakupa ushauri kulingana na changamoto ambazo wasomaji wenzetu wametuandikia kwamba zinawakwamisha.

Leo tunakwenda kuangalia changamoto kubwa ambayo wengi wamekuwa wanaipigia kelele. Changamoto hiyo ni kukosa mtaji wa kuingia kwenye biashara. Kila siku kuna watu wengi wanasema wanataka kuingia kwenye biashara ila hawana mitaji.

Leo tunakwenda kuangalia kama kweli hii ni changamoto ya kumzuia mtu na kuona hatua za kuchukua ili ukosefu wa mtaji usiwe changamoto.

Kabla hatujaangalia kipi cha kufanya, tupate maoni ya wasomaji wenzetu;

Changamoto ni ukosefu wa mtaji na aina gani ya biashara nianze. – Abel M.N

Sina Mtaji Na Nimezaliwa Katika Familia Masikini. Hakuna Wa kuniwezesha Kufikia Malengo. – Nelson H.M

Changamoto kubwa ni mtaji, nina mawazo mengi na ya kujenga lakini mtaji ndio kikwazo, yaani hata ule mdogo kwangu ni changamoto kuupata. – Jenifer M.M

Changamoto kubwa ni kukosa mtaji. Esther C.M

Kama ambavyo wametuandikia wengi, ukosefu wa mtaji unaonekana kuwa kikwazo kikubwa kwa watu kuingia kwenye biashara.

Lakini ukweli ni kwamba, mtaji haujawahi kuwa kikwazo kikubwa kwa wale ambao wameingia kwenye biashara na kufanikiwa.

Wapo watu wengi ambao wameanza biashara bila ya kuwa na mtaji au kwa mtaji kidogo na wameweza kupata mafanikio makubwa sana.

Leo nakwenda kukushirikisha njia za kuweza kuanza biashara na kufanikiwa hata kama una mtaji kabisa.

Lakini kabla hatujaangalia njia hizo, kwanza tuanze na mtaji kwanza, mtaji ni nini na unawezaje kutumia mitaji mingine uliyonayo katika biashara.

Wengi wanaozungumzia mtaji kwenye biashara, wanazungumzia kitu kimoja pekee ambacho ni fedha. Lakini mtaji kwenye biashara siyo fedha pekee, ndivyo fedha ni muhimu sana, lakini kama huna fedha haimaanishi huwezi kufanya biashara.

Kuna mitaji mingine muhimu sana ambayo unaweza kuitumia kwa mafanikio makubwa kwenye biashara. Ujuzi ulionao ni mtaji mkubwa sana ambao unaweza kuutumia kuingia kwenye biashara. Uzoefu ambao umeupata maeneo mbalimbali ya maisha yako ni mtaji mzuri pia. Watu unawajua na wanaokujua ni mtaji pia ambao ukiweza kuutumia vizuri utakuwezesha kupiga hatua. Uaminifu wako na mahusiano mazuri na wengine ni mtaji ambao unaweza kukusaidia sana.

Hiyo ni baadhi tu ya aina nyingi za mitaji unazoweza kutumia kuanza biashara yako na kufanikiwa zaidi. Nina imani umepata picha na unaweza kuorodhesha aina nyingine za mtaji ulizonazo na kuona jinsi unavyoweza kuzitumia kupiga hatua.

Zifuatazo ni njia unazoweza kutumia kuingia kwenye biashara hata kama huna mtaji au mtaji ni kidogo.

  1. Anza na kutoa huduma, kupitia ujuzi au uzoefu ulionao.

Watu wengi wanapofikiria biashara, wanafikiria biashara za bidhaa na biashara kubwa. Ni njia nzuri ya kufikiria, lakini hutaweza kufika huko kama hutaanzia mahali fulani.

Kama huna mtaji mkubwa wa fedha wa kukuwezesha kuwa na biashara kubwa ya bidhaa, unaweza kuanza na biashara ya huduma. Kwa biashara hii, unatoa muda, ujuzi na uzoefu wako katika kuwasaidia wengine. Biashara nyingi za huduma hazihitaji uwe hata na eneo la biashara, hasa kwa zama hizi za mtandao wa intaneti na mitandao ya kijamii.

Unachohitaji ni kuangalia ni kitu gani wewe unaweza kufanya au kuwasaidia watu kufanya, kisha angalia ni watu gani wanahitaji kitu hicho na unawezaje kuwafikia. Hapa unachohitaji ni ujuzi, uzoefu na muda.

Biashara unazoweza kufanya kwenye huduma ni ushauri, uandishi, ufundishaji, usimamiaji na hata kuajiriwa na wengine kulingana na kile unachofanya.

Unapoanza na biashara za aina hii, usipoteze lengo lako la biashara kubwa zaidi baadaye, hivyo chochote unachopata unakitumia kupiga hatua zaidi.

  1. Watumie watu wanakujua na kukuamini kupata fedha za kuanza biashara.

Linapokuja swala la mtaji wa fedha kwenye biashara, kuna makundi mawili ya watu, kundi la kwanza ni watu wanaotaka kuingia kwenye biashara lakini hawana mtaji, na kundi la pili ni watu ambao wana mtaji ila hawajui biashara gani wafanye, au hawana muda wa kufanya na kusimamia biashara zao.

Ni wajibu wako kuwajua watu wa kundi la pili kwenye maisha yako. Waangalie watu wote unaowajua na wanaokujua, ambao wanakuamini kulingana na mahusiano yenu ya siku za nyuma. Hawa waendee na wazo lako la biashara na kwa namna gani unahitaji ushiriki wao. Kama ni ushirika au wao kukuwezesha wewe.

Hili linakuhitaji wewe uwe ni mtu mwaminifu, mtu unayeweza kutegemewa kufanya kile unachosema unafanya. Hivyo kama hujatengeneza mazingira ya aina hii, anza kuyatengeneza sasa.

  1. Anza na aina za biashara ambazo hazihitaji mitaji mikubwa.

Kuna aina za biashara ambazo hazihitaji mitaji mikubwa, ila zinahitaji nguvu zako sana. kwa mfano biashara ya kutembeza vitu kwa watu, kama vitu vya ndani, nguo na huduma nyingine muhimu. Biashara za aina hii unahitaji kuwa tayari kuweka juhudi kubwa. Pia usione aibu kwamba watu wanakuchukuliaje, hasa pale unapokuwa una elimu kubwa. Unahitaji kujijali kwanza wewe kabla hujajali wengine watasema au kukuchukuliaje.

  1. Fanya mauzo kwa kamisheni kutengeneza mtaji.

Ni kweli kwamba kwa sasa ajira zimekuwa ngumu, lakini watu bado wanataka bidhaa na huduma zao ziuzwe. Hivyo ukiweza kuuza bidhaa na huduma za wengine na wao wakakulipa kwa kamisheni, kulingana na mauzo yako, itakusaidia kupata mahali pa kuanzia.

Yapo makampuni mengi yanayotoa nafasi ya watu kuwa wauzaji wa bidhaa na huduma zao na kuwalipa kwa kamisheni. Na pia mtu yeyote mwenye biashara, atakuwa tayari kukupa fursa hiyo kama utakuwa mtu mwaminifu na wa kujituma.

  1. Fanya biashara ya mtandao (network marketing)

Huu ni mfumo wa biashara ambapo unauza bidhaa na huduma za makampuni na wewe unalipwa kulingana na faida unayotengeneza. Uzuri wa mfumo huu ni kwamba malipo yake yanaweza kuwa makubwa kulingana na kazi unayofanya. Pia unaweza kupata kamisheni kutokana na kazi za watu wengine, na siyo kazi uliyofanya wewe tu.

Biashara ya mtandao ni sehemu ambayo nimekuwa nawashauri watu waanzie kama hawana mtaji au uzoefu wa biashara. Kupitia mifumo hii mtu anajifunza mambo mengi kuhusu biashara.

Kupata maelezo zaidi na kujua jinsi ya kuchagua biashara ipi ya mtandao mtu afanye, kuna kitabu nimeandika kinaitwa IJUE BIASHARA YA MTANDAO, kipate na ukisome, kitakusaidia sana. kukipata tuma ujumbe kwa wasap namba 0755 953 887.

NETWORK MARKETING

Usikubali kitu chochote kikuzuie wewe kuingia kwenye biashara, kwa sababu tunaishi kwenye zama ambazo kila kikwazo cha kibiashara kimeshatatuliwa. Tumia kila fursa iliyopo mbele yako kuhakikisha unapiga hatua kwenye biashara na kuweza kufanikiwa.

Nakutakia utekelezaji mwema wa yale ambayo umejifunza,

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TOA CHANGAMOTO YAKO USHAURIWE

Kama una changamoto ambayo inakuzuia kufikia malengo yako unaweza kuitoa kwa kubonyeza maandishi haya na kujaza fomu. Changamoto yako inaweza kuwa moja ya makala zijazo kila siku ya jumatatu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog