Kadiri siku zinavyokwenda, ndivyo uwezo wa watu kufikia maamuzi yao wenyewe unavyozidi kuwa mgumu. Hii inatokana na wingi wa machaguo, wingi wa maarifa na taarifa na pia wingi wa ushauri ambao mtu anaweza kupata juu ya jambo lolote lile.
Unapotaka kufanya jambo lolote na ukaanza kutafuta taarifa na maarifa, utayapata mengi sana, yapo yatakayokuonesha ni kitu kizuri kufanya na yapo yatakayokuonesha ni kitu kibaya kufanya.

Ukiomba ushauri ndiyo kabisa utapata ushauri wa kila aina, wapo watakaokuambia ni sawa unavyofanya na wapo watakaokuambia unafanya makosa au utashindwa.
Kwa akili ya kawaida, tungetegemea wingi wa maarifa, taarifa na hata ushauri kurahisisha kufikia maamuzi, lakini matokeo ni kinyume chake. Wingi huu unachelewesha maamuzi. Mtu anatumia muda mwingi kuchambua mengi anayopata na mwishowe anakuwa njia panda asijue hatua ipi achukue.
SOMA; UKURASA WA 52; Epuka Miluzi Mingine…
Hii ni hali ambayo imewarudisha wengi nyuma na kuwazuia wengi kupiga hatua.
Kuepukana na hali hii, jipe wajibu wa kufanya maamuzi yako wewe mwenyewe. Pamoja na maarifa, taarifa na ushauri utakaopokea kutoka kwa wengine, lazima uweze kukaa chini na kufanya maamuzi yako mwenyewe. Lazima ufanye maamuzi ukijua unaweza kukosea pia, na kuwa tayari kubeba makosa yako.
Ukitaka usubiri mpaka upate maarifa au ushauri ambao hautakuwa na makosa kabisa, utashindwa kufanya maamuzi na utashindwa kupiga hatua. Kuwa tayari kufanya maamuzi yako, ambapo pia unaweza kukosea lakini angalau utachukua hatua fulani kuliko kusubiri na kuchambua wingi wa maarifa, taarifa na ushauri.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog