Maisha ni magumu, kwa kila kiumbe hai kilichopo hapa duniani kwa sababu kila kiumbe kina changamoto zake.

Lakini pamoja na ugumu huu wa maisha, maisha hayakuandaliwa kuwa mateso. Kila ugumu na changamoto ambayo kiumbe hai kinakumbana nayo, asili imeandaa mazingira ya kiumbe huyo kupambana na changamoto hiyo.

Kwa mfano, miti inayoota kwenye eneo la ukame, huwa ina majani madogo sana, na wakati mwingine miiba pekee. Hii ni njia ya kupunguza upotevu wa maji, ambayo ni adimu kwenye ukame, na pia kuzuia majani yake yasiliwe na wanyama na hivyo uhai wake ukaisha.

Maisha Hayajawahi

Viumbe wanaoishi kwenye maji ya bahari ambayo yana chumvi kali, miili yao ina kiwango kikubwa cha chumvi kuliko viumbe wengine.

Kadhalika kwetu sisi binadamu, ugumu na changamoto zozote ambazo tunakutana nazo, tunayo namna ya kuzitatua na maisha yetu yakaenda vizuri, bila ya mateso.

Hakuna mtu anapaswa kwenda na mateso maisha yake yote, maisha hayo hayatakuwa na maana, kwa sababu hilo halikuwa kusudi la maisha.

Changamoto au ugumu wowote ambao unaupitia kwenye maisha yako, kuna njia za kuutatua, kuna namna unaweza kuzivuka, na muhimu zaidi, mwili wako umeandaliwa vyema katika kukuwezesha kuvuka kila changamoto unayokutana nayo.

SOMA; UKURASA WA 938; Nyakati Ngumu Ndiyo Za Kutengeneza Maana.

Changamoto kubwa ni kwamba, wengi huwa hawajui kile kilichopo ndani yao, huwa hawajichunguzi na kujijua kiasi cha kuweza kupambana na magumu wanayopitia. Wengi wakishakutana na magumu wanakubaliana nayo na kuona maisha yao ni ya mateso mpaka siku ya kufa. Hii siyo sahihi, hakuna anayepaswa kuteseka mpaka anapokufa, wengi wanajiamulia tu kuteseka mpaka kifo.

Jijue wewe mwenyewe, jua uwezo mkubwa uliopo ndani yako wa kuweza kupambana na chochote na unapokutana na magumu au changamoto, yatatue hatua kwa hatua. Maisha yatakuwa mazuri na yenye furaha, hata kama una magumu na changamoto. Kwa sababu kadiri unavyozitatua, ndivyo unavyokuwa bora zaidi.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog