Kadiri unavyofanikiwa kwenye kazi, biashara na hata maisha yako kwa ujumla, ndivyo unavyowavutia watu wengi zaidi kutaka kushirikiana na wewe. Unaweza kuwavutia kama wafanyakazi ambao wanakusaidia kwenye majukumu yako. Pia unaweza kuwavutia kama watu wanaohitaji kushirikiana na wewe katika yale unayofanya.

Sasa kumekuwa na tatizo moja kubwa, watu wanapoona umefanikiwa wanafikiri mafanikio ni rahisi, na wewe unastahili kuwapa mafanikio yako. Na hivyo watu hupenda kutumia maneno zaidi ili kukushawishi wewe uwape kile ambacho wanataka kupata.

Kila Mtu

Ukiwa mtu wa kuamini maneno hayo, kila wakati utaishia kuangushwa na kupoteza kwa sababu watu ni wazuri sana katika maneno. Watu wanaweza kuongea sana, wanaweza kupanga sana na wanaweza kukufanya uone mambo yatakwenda vizuri kabisa. Lakini pale unapowaamini kwa maneno yao, ndipo unapopoteza.

Badala ya kuwaamini watu kwa maneno yao, wape nafasi ya kukuonesha kwa vitendo. Chochote ambacho mtu anakuambia anaweza kufanya au anaweza kukusaidia ukapiga hatua zaidi, mpe nafasi ya kukuonesha kwa vitendo anafanyaje. Hapo utaweza kujionea mwenyewe iwapo maneno anayosema mtu ni kweli au la. Na hili pia litakupunguzia watu wanaofikiri mafanikio ni rahisi wasikusumbue, kwa sababu watu wakishajua unataka waoneshe kwa vitendo, wale wababaishaji wanakimbia wenyewe.

Ni mtu amekuja kwako na wazo bora la kuweza kupiga hatua zaidi kwako na kwake pia? Mwambie akuoneshe kipi amewahi kufanya ambacho kinaweza kukushawishi uamini maneno yake. Au kama ndiyo amepata wazo na hajawahi kufanya, basi mpe nafasi ya yeye kufanya kwanza kisha ndiyo aje kwako na matokeo.

Ni mtu anakuambia kwa elimu na uzoefu alionao anastahili kupata malipo makubwa zaidi kwenye kazi anazokufanyia? Vizuri, mwambie aoneshe ni kwa namna gani anastahili kipato hicho kikubwa zaidi. Aweke juhudi ambazo zinaongeza thamani zaidi ambapo wewe unaweza kumwongezea kipato chake zaidi.

SOMA; UKURASA WA 433; Hamasa Ni Nzuri Lakini…

Ukitumia njia hii ya kuwataka watu wakuoneshe kwa vitendo, utawaepuka wababaishaji wengi sana. Na unahitaji kuwa na msimamo sana kwenye hilo kwa sababu kuna watu wana maneno ambayo ni mazuri na unaweza kujishawishi ujaribu kuona kama ni kweli. Ukijaribu unapoteza.

Kadhalika hata kwa mtu anayekuambia kuna fursa kubwa ya kupata fedha ambayo ameipata, mwambie akuoneshe kwanza yeye ni kiasi gani cha fedha ametengeneza kwenye fursa hiyo. Na kama bado hajatengeneza, basi mwambie atengeneze kisha aje kwako na ushahidi.

Ukienda na msimamo huu, kwa hakika utaepuka hata kutapeliwa au kupotezewa muda kwa mambo yasiyo ya kweli.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog