Habari za leo rafiki yangu?

Inapotajwa fedha, basi kila mtu kuna picha ambayo anaipata kwenye akili yake. Wapo ambao wanapata picha nzuri ya kwamba fedha ni kitu kizuri kinachowezesha maisha kwenda vizuri. Lakini pia wapo wanaopata picha mbaya ya kwamba fedha ni kitu kinachowaletea mateso kwenye maisha yao. Kwa kuwa kila mtu anapata kile anachofikiri kwa muda mrefu, wanaopata picha kwamba fedha ni nzuri wanazidi kuona uzuri, wakati wanaoona ni mbaya wanazidi kuona ubaya.

Kila mtu anatumia fedha kwenye maisha yake, lakini ni wachache sana ambao wana uelewa wa ndani kuhusu fedha. Na hii ni kwa sababu, tumekulia kwenye jamii ambazo zinatufundisha kitu kimoja, unafanya kazi, unalipwa fedha, unazitumia mpaka ziishe huku ukisubiri malipo mengine. Na hapo katikati, wakati unasubiri fedha nyingine zitoke, ukitaka kitu unaweza kukopa, halafu fedha zikitoka utalipa. Hii ndiyo hadithi ambayo karibu kila mmoja wetu ameona wazazi na walezi wake wakiishi na yeye kuendelea kuiishi.

KWA NINI SIYO TAJIRI

Ni watu wachache sana ambao wanakaa chini na kusema hivi kweli ndivyo mambo yanavyopaswa kwenda hivi kwenye swala la fedha? Kwa sababu huu mzunguko wa fanya kazi, pata fedha, tumia, kopa, subiri fedha nyingine ni aina ya utumwa ambao mtu anakuwa amejitengenezea.

Eneo la fedha ni eneo ambalo nimekuwa naliandikia mara kwa mara kwa sababu watu wengi sana hawajapata nafasi ya kuelewa fedha kwa undani. Pia nimewahi kuendesha semina ya ELIMU YA MSINGI YA FEDHA, ambapo tulijifunza kuhusu fedha kwa undani kabisa ambapo masomo yote yapo kwenye KISIMA CHA MAARIFA.

Leo nakwenda kukushirikisha tofauti ya fedha kwenye kuwekeza, kutumia na kukopa, ili uone mwenyewe kila hatua unayochukua ni kwa namna gani inakuathiri wewe na kuathiri kesho yako.

Katika kukuonesha tofauti hii, nakwenda kutumia mfano wa jeshi, na fedha uliyonayo ndiyo jeshi lako, ambalo unalitumia kupigana vita ya kiuchumi na mafanikio.

Sasa kama tunavyojua, kwenye fedha kuna mambo makuu manne, kupata fedha, kutumia fedha, kuweka akiba na kuwekeza na kukopa fedha.

Tukitumia mfano wetu wa jeshi, tunaweza kuelezea mambo matatu kati ya hayo manne kama ifuatavyo;

Unapowekeza fedha ni sawa na kukuza jeshi lako, unapata fedha nyingi zaidi. Unaifanya fedha yako ikufanyie kazi na kuzalisha fedha zaidi. Hapa unaongeza ukubwa wa jeshi lako na kuwa na nguvu ya kupigana vita ya uchumi na mafanikio.

Unapotumia fedha, maana yake unapoteza fedha, unapunguza jeshi lako na unakosa nguvu ya kupigana vita ya uchumi na mafanikio. Kadiri unavyotumia fedha ndivyo unavyobaki na fedha kidogo, ndivyo unavyokuwa dhaifu kifedha. Na kama unatumia kuliko unavyotengeneza basi ndiyo upo kwenye hatari kubwa zaidi. Kama huwekezi kabisa basi unajiweka kwenye mazingira ya kuwa mtumwa wa fedha maisha yako yote.

Unapokopa fedha, unatumia fedha zako kuwaongezea wengine fedha zaidi. Yaani unatumia jeshi lako kuimarisha majeshi ya watu wengine. Wewe unapoteza fedha na wengine wanapata fedha zaidi kupitia wewe. unapokopa fedha unalipa kwa riba, unalipa nyingi kuliko uliyokopa, na hapo ndipo unapopoteza fedha zako. Na kama umekopa kwa ajili ya matumizi, yaani hapo unakuwa umeamua kuchukua fedha zako na kuzitupa au kuchoma moto.

Nafikiri kwa mifano hii mitatu unaona jinsi gani maamuzi yako ya matumizi ya fedha yanavyoweza kukujenga au kukubomoa zaidi, hasa kwenye uwezo wako wa kupiga hatua na kufanikiwa.

Hivyo rafiki yangu, kila unapopata fedha, kabla hujafanya chochote, kabla hujafikiria matumizi ya aina yoyote, kwanza wekeza. Weka pembeni fungu la uwekezaji, kwa sababu hili ndiyo muhimu, hili ndiyo litakalokuwezesha kuwa na uhuru zaidi baadaye.

Ukishaweka pembeni fungu la uwekezaji, hapo sasa ndiyo unaruhusiwa kufanya matumizi. Unafanya matumizi yale ambayo ni ya msingi na muhimu zaidi kwako.

Lakini unapofanya matumizi yako, kuwa makini sana usivuke mstari. Kamwe kamwe usikope fedha kwa ajili ya matumizi, kama fedha zimeisha na matumizi bado yapo basi angalia utaratibu mwingine, wa kuacha matumizi hayo kama siyo muhimu sana, au wa kutafuta kipato cha ziada ili kumudu matumizi hayo. Kamwe usikope, usikope kutumia, unakuwa unachagua kupoteza fedha, unatumia fedha zako kujenga majeshi ya wengine.

Mambo haya yanahitaji kitu kimoja kutoka kwako, NIDHAMU. Bila ya nidhamu utasoma hapa na kufurahi, na kuona ukombozi wako wa kifedha umeshaupata, lakini unapozishika fedha, unaanza kukutana na matumizi, mara dharura inatokea, mtu anaumwa, kitu kinaharibika, ukija kustuka fedha zimeshaisha na bado una mahitaji, unajiambia nikikopa kidogo siyo shida. Na hapo ndipo unapoingia kwenye shimo kubwa ambalo linakuwa gereza lako kifedha.

Weka juhudi kwenye kuhakikisha una njia nyingi za kukuingizia kipato, kuwa na mifereji mingi ya kipato, itakusaidia sana. ukishapata fedha, anza kwa kuweka pembeni fungu la kuwekeza, weka pia fungu la dharura. Ukishaweka pembeni kile kiasi cha kuwekeza na dharura, fanya matumizi. Lakini matumizi yawe na kikomo. Na kamwe usikope. USIKOPE. Kwa msisitizo zaidi usikope, kuwa na nidhamu kwenye fedha zako na epuka mikopo. Kama tayari upo kwenye mikopo, usiendelee kukopa na lipa madeni hayo ili kuwa huru.

Kujifunza kwa kina kuhusu fedha, karibu ujiunge na KISIMA CHA MAARIFA. Kwenye KISIMA yapo mafunzo ya semina ya ELIMU YA MSINGI YA FEDHA ambayo yatakupa misingi yote muhimu ya fedha, kuanzia kuipata, kuitumia, kuwekeza na hata kufikia utajiri mkubwa.

Karibu sana kwenye KISIMA CHA MAARIFA, kujiunga nitumie ujumbe kwa njia ya wasap 0717 396 253 na nitakupa maelekezo ya kujiunga.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA www.kisimachamaarifa.co.tz/kujiandikisha

Kupata huduma za Ukocha; www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha

Kujiunga na Kundi la kusoma vitabu; www.amkamtanzania.com/kurasa

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog