Rafiki yangu mpendwa,
Karibu kwenye makala ya ushauri wa changamoto mbalimbali tunazokutana nazo na zinazotuzuia kupiga hatua kubwa kwa mafanikio yetu. Kila hatua tunayopiga kwenye maisha yetu tunakutana na changamoto mpya, hivyo kutamani changamoto zisiwepo ni kutokutaka mafanikio.
Leo tunakwenda kuangalia changamoto ya kuchukua mkopo wa biashara kimakosa na baadaye ukakusababishia hasara kubwa na biashara kufa.
Watu wengi wamekuwa wanakimbilia kuchukua mikopo ya kibiashara bila ya kufanya tathmini sahihi ya uwezo wa biashara kulipa mkopo ambao inachukua. Kinachotokea ni badala ya mkopo kuikuza biashara, unapelekea biashara kufa kabisa.
Msomaji mwenzetu ametuandikia haya kwa upande wa changamoto hii;
“Madeni ya benki, sikufanya biashara kiufanisi ikanifilisi kiasi kwamba nimeanza moja.” – E. F. Mpelumbe.
Unapogundua kwamba umefanya makosa kwenye maisha yako, hatua ya kwanza kuchukua ni kuacha kuendelea kufanya makosa hayo.
Na nimekuwa natumia mfano huu, kama umejikuta kwamba tayari upo kwenye shimo, hatua ya kwanza kuchukua ni kuacha kuchimba, maana kama upo kwenye shimo na unaendelea kuchimba, unazidi kupotea.
Hivyo unapojikuta kwenye madeni, hatua ya kwanza ni kuacha kabisa kukopa, kwa sababu wengi waliopo kwenye madeni, huwa wanakimbilia kukopa zaidi wakifikiri ndiyo njia itakayowatoa pale walipo, kitu ambacho kinawapoteza zaidi.
Hivyo acha mara moja kukopa tena, na ondoa mpango wa kukopa kwa kipindi ambacho unaijenga biashara yako upya.
Baada ya kuacha kucha kukopa, sasa kuna mtaji muhimu sana unaopaswa kuutumia sawasawa, tunauita huu ni mtaji wa jasho. Hapa unahitaji kuweka kazi kubwa sana, unapaswa kujisukuma na kwa njia nyingine, unapaswa kujiadhibu kwa makosa uliyofanya mpaka yakapelekea biashara kushindwa.
Kwa sasa huhitaji kuanza kujiuliza kama unafanya kazi sana au unapaswa kupata muda wa kupumzika, unapaswa kuweka muda mwingi kwenye biashara yako. Fanya kila kinachopaswa kufanya, na nenda hatua ya ziada kwenye kila unachofanya.
SOMA; Tofauti Ya Fedha Kwenye Uwekezaji, Matumizi Na Kukopa.
Ikuze biashara yako kwa kuanzia chini kabisa kwa kuweka jasho. Ongeza wateja wa biashara yako kila siku, wafikie wengi zaidi kwa kila njia unayoweza, hata kama itabidi kumfuata mtu nyumba kwa nyumba.
Rudisha sehemu kubwa ya faida ya biashara yako kwenye kukuza biashara. Hili ndiyo eneo muhimu sana ambalo wengi wanakosea nakuteleza. Wengi huwa hata hawajui faida halisi ya biashara zao ni kiasi gani. Wanachofanya ni wakiona mauzo wanajua ndiyo fedha zao.
Unachopaswa kujua ni kwamba mauzo ya biashara siyo fedha yako, bali ni fedha ya biashara. Fedha yako kwenye biashara ni faida unayoipata, na faida ni baada ya kutoa gharama zote za biashara, pamoja na kujilipa wewe mwenyewe. Ile inayobaki ndiyo faida ya biashara, na kwa kipindi kigumu kama hiki cha biashara yako, rudisha faida yote kwenye kukuza zaidi biashara yako.
Usitoe fedha kwenye biashara kwa matumizi yoyote nje ya biashara yako. Achana na matumizi yoyote ambayo siyo ya muhimu kwa biashara, kwa sasa biashara inahitaji msaada mkubwa ili kuweza kukua.
Mwisho, weka nguvu zaidi kwenye maeneo ambayo yanakua zaidi kwenye biashara yako. Kwa jinsi unavyoijua biashara yako, kuna maeneo ambayo yanatoka zaidi kuliko maeneo mengine. Sasa unahitaji kukazana na maeneo hayo kwa kipindi hiki kigumu. Usifanye yale ambayo unapenda wewe, bali fanya yale ambayo wanapenda wateja.
Nakutakia utekelezaji mwema wa yale ambayo umejifunza,
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
TOA CHANGAMOTO YAKO USHAURIWE
Kama una changamoto ambayo inakuzuia kufikia malengo yako unaweza kuitoa kwa kubonyeza maandishi haya na kujaza fomu. Changamoto yako inaweza kuwa moja ya makala zijazo kila siku ya jumatatu.
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog