Usipokuwa makini utashangaa siku inaanza na kuisha huku hujapata nafasi ya kufanya lolote muhimu ulilotaka kufanya. Unaweza kuwa na mipango mizuri sana ya siku yako, lakini siku ikaanza na kuisha na usione muda wa kufanya yale muhimu uliyopanga.

Hii yote inayokana na namna mambo ya kufanya yanavyozidi kuwa mengi huku muda wetu ukiwa ni ule ule. Usumbufu pia umekuwa mwingi, japo siyo rahisi kuuona kama usumbufu, tunauona kama mawasiliano na kuhabarika au kwenda na wakati.

Kwa kuwa mambo haya mengi yanapambana kupata muda wako, pamoja na watu pia, njia pekee ya kulinda muda wako na kuweza kufanya yale muhimu zaidi ni kutenga baadhi ya masaa ya siku yako na kuyafanya kuwa matakatifu.

Mitandao

Unaweza kuanza na saa moja kwenye siku yako, saa hiyo unaitangaza kuwa takatifu kwako, kwa kuifanya kuwa saa muhimu kwako ya kufanya yale ambayo ni muhimu. Katika saa hiyo usiruhusu kitu kingine chochote ambacho siyo muhimu, hata kama umeshawishika kiasi gani. Utakifanya lakini siyo kwa muda huo uliotenga ambao ni takatifu kwako.

Itapendeza zaidi kama katika saa hiyo hutakuwa hata na simu, iwe umeizima au uko mbali nayo, kwa sababu hutaki chochote kikuondoe kwenye saa hiyo muhimu kwako.

Je unafanya nini kwenye saa hiyo takatifu kwako?

Kwanza kabisa unasali au kufanya tahajudi kulingana na kile ambacho ni muhimu kwako. Huu ni wakati wa kutulia na kuyatafakari maisha yako na pia kutoa shukrani kwa kila ulichonacho kwenye maisha yako.

SOMA; Mbinu za kisaikolijia za kistoa – KUTAFAKARI/TAHAJUDI.

Pili unaandika yale muhimu ya maisha yako, unaandika malengo na mipango yako, unaandika ndoto zako, unatengeneza na kupitia taswira ya maisha unayoyataka. Hili ni zoezi ambalo linaichangamsha akili yako ili iweze kukuonesha fursa za kufika kule unakotaka kufika.

Tatu unajifunza, kwa kujisomea vitabu ambavyo ni vizuri na muhimu kwako kwenye kupiga hatua. Hapa unatulia na kusoma kitabu ambapo utapata maarifa unayokwenda kufanyia kazi mara moja.

Hayo matatu ya msingi kila mtu anapaswa kuyafanya kwenye saa yake takatifu, kila siku.

Yapo mengine ambayo mtu unaweza kuyafanya, kulingana na shughuli zako. Mfano unaweza kutumia muda huo kuandika kama wewe ni mwandishi. Unaweza pia kutumia muda huo kufanya mazoezi. Kadiri unavyokuwa na mengi ya kufanya kwenye wakati huu, utahitaji kuwa na muda mrefu zaidi.

Muda mzuri wa kutenga saa hii takatifu kwako ni asubuhi na mapema. Huu ni muda ambao hakuna usumbufu mkubwa kwako na hivyo unakuwa na nafasi ya kuweza kufanya mengi kwa muda mfupi. Pia unakuwa na nguvu kimwili na kiakili kwa sababu ulipumzika vya kutosha.

Usikubali masaa yote 24 ya siku yapotelee kwa wengine, hata kama unalipwa kiasi gani kwa masaa hayo. Tenga angalau saa moja na ifanye saa takatifu kwako, saa ya kujijenga wewe, saa ya kukuwezesha kupiga hatua zaidi.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog