Habari za asubuhi ya leo rafiki yangu?

Hongera kwa nafasi nzuri ya leo, nafasi ya kipekee kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili tuweze kupata matokeo bora sana.

Karibu kwenye makala hizi za ushauri wa changamoto mbalimbali ambazo zinatuzuia kufikia mafanikio makubwa kwenye maisha yetu. Kama ambavyo nimekuwa nakuambia mara zote, changamoto ni sehemu ya safari hii, hivyo njia bora siyo kuzikimbia, bali kuzitatua.

Pia hakuna changamoto ambayo haina utatuzi kabisa, ukiwa mtulivu na unayejia ni wapi unapotaka kufika, kila changamoto ina utatuzi na kama haina basi kuna njia ya kuizuia isiwe kikwazo kwako.

Leo tunakwenda kuangalia changamoto ya kukosekana kwa uaminifu kwa watu ambao unashirikiana nao kwenye kazi au biashara unazofanya. Hii ni changamoto kubwa kwa sababu wewe unaweza kuwa unaweka juhudi kubwa ili ufanikiwe, wakati wenzako wanaweka juhudi kubwa ili ushindwe. Usipokuwa na njia sahihi za kutatua changamoto hii, utaishia kuanguka, kugombana na wengine na kuharibu mahusiano yako.

Kabla hatujaangalia hatua zipi ambazo mtu anaweza kuchukua katika changamoto hii, tupate maoni ya msomaji mwenzetu aliyetuandikia kuhusu changamoto hii;

Ya kwanza ni unafiki. Pili mtu ninayefanya naye kazi ni muongo. Je Nitafute mbinu nyingine? Tatu dhuluma, kitu hicho narudi nyuma sana. – Kizimba S.

Kama alivyotuandikia mwenzetu hapo, mambo hayo matatu ni kikwazo kikubwa sana kwa mafanikio kwenye kazi au biashara. Pale ambapo watu wanakuwa na unafiki, uongo na dhuluma, hakuna mtu anaweza kupiga hatua. Kinachotokea ni watu kurudishana nyuma na mwisho wa siku kila mtu anaumia.

Je mtu unawezaje kuondokana na hali hizo? Unawezaje kuhakikisha watu unaofanya nao kazi au biashara siyo wanafiki, waongo na watu wa dhuluma?

Jibu ninaloweza kukupa hapa ni moja, watu wanakupa kile ambacho unakubaliana nacho, kile ambacho unakivumilia.

Iko hivi rafiki, watu watakufania unafiki, watakudanganya na kukudhulumu kama wewe unakubaliana nao kwenye mambo hayo, kama unaweza kuyavumilia basi watayafanya. Na wataendelea kuyafanya mpaka pale wewe utakapokataa na kusema inatosha. Pale utakaposhindwa kuvumilia hayo mambo ambayo wengine wanayafanya kwako, ndipo na wao wanapoacha kuyafanya.

Hivyo kwa hali uliyonayo, ya watu kuwa wanafiki, waongo na kukudhulumu, ni kwa sababu hujawa na ujasiri wa kuwakataza na kuwazuia kufanya hivyo, umekuwa unawavumilia kwa hayo wanayofanya, na wao wanaendelea kufanya, kwa sababu wanajua utavumilia.

SOMA; Sababu Kubwa Inayopelekea Watu Wengi Kutofikia Malengo Wanayojiwekea Kila Mwanzo Wa Mwaka.

Unachopaswa kufanya ni kukataa kabisa hayo mambo, usikubali kwa namna yoyote ile kuvumilia au kukubaliana na mtu pale anapoleta unafiki, uongo na dhuluma.

Mtu anapokuwa mnafiki, mweleze wazi kwamba unajua anachofanya na hupendezwi nacho. Usione aibu wala kufikiria mtu atakuchukuliaje, kama jambo linakuudhi mweleze wazi jinsi lilivyo na kwa nini hulifurahii na wala hutaweza kulivumilia.

Kama mtu amekudanganya na ukaujua ukweli, mweleze wazi kwamba umeujua ukweli, na hupendi uongo. Mwambie wazi ya kwamba hamtaweza kwenda pamoja kama mtu ataendelea na uongo alionao. Mwambie kwamba hutavumilia tena uongo.

Na kama mtu amekudhulumu, mweleze wazi kwamba alichokifanya hujapendezwa nacho na hutavumilia tena tabia ya aina hiyo katika mambo mnayoendelea kufanya.

Sasa baada ya kuwa umemweleza mtu wazi kuhusu kile anachofanya, iwapo atarudia tena chukua hatua mara moja, acha kabisa kuihusisha na mtu huyo kwenye kazi au biashara. Achana na mtu huyo kwa sababu ataendelea kukuumiza na kukurudisha nyuma, kitu ambacho wewe huwezi kukubaliana nacho.

Usione aibu wala kumwonea huruma mtu wa aina hiyo, usitake kuendelea naye kwa kuamini atabadilika kwa sababu wewe umemwambia abadilike. Huwezi kumbadili mtu yeyote, na ni watu wachache sana wanaoweza kubadilika. Badala ya kukazana kubadili watu, ni bora ukatumia muda huo kutafuta wale ambao tayari wana tabia nzuri na zinazoendana na wewe. hawa mtaweza kwenda pamoja.

Wakati unafanya yote haya, hakikisha wewe siyo mnafiki, siyo mwongo na hudhulumu wengine. Kwa sababu kama hizi ni tabia ambazo wewe unazo, hata ukiachana na hao unaoamini wanakufanyia hivyo, utakaokutana nao wapya nao watakuwa na tabia hizo pia. Sheria ya asili ni kwamba huwa tunavutia kile ambacho sisi tunacho, hivyo mara nyingi utajikuta unaishia kuwa na watu wanaoendana na wewe.

Hivyo hakikisha wewe mwenyewe una tabia nzuri katika mahusiano yako na wengine, siyo mnafiki, siyo mwongo na pia siyo mtu wa dhuluma. Baada ya kuhakikisha hilo kwako, usimvumilie kabisa mtu ambaye ana tabia za aina hiyo. kuwa mtu wa kutoa nafasi chache sana kwa watu ambao wanaonesha tabia usizokubaliana nazo. Kama hawataweza kwenda kwa vile unavyothamini wewe, ni vyema ukakaa nao mbali.

Mwisho kabisa usiogope kwamba utakosa watu wa kushirikiana nao kwenye kazi, biashara na hata maisha. Watu wapo wengi mno, tena wenye tabia nzuri sana, wanashindwa kushirikiana na wewe kwa sababu umezungukwa na watu wenye tabia mbaya. Ukishaondokana na watu hao wenye tabia mbaya, utatoa nafasi kwa wale wenye tabia nzuri muweze kushirikiana.

MIMI NI MSHINDI

Nakutakia utekelezaji mwema wa yale ambayo umejifunza,

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TOA CHANGAMOTO YAKO USHAURIWE

Kama una changamoto ambayo inakuzuia kufikia malengo yako unaweza kuitoa kwa kubonyeza maandishi haya na kujaza fomu. Changamoto yako inaweza kuwa moja ya makala zijazo kila siku ya jumatatu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog