And thou wilt give thyself relief, if thou doest every act of thy life as if it were the last – Marcus Aurelius
Ni siku mpya, siku ya kipekee sana kwetu ambapo tumepata nafasi nyingine nzuri ya kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Tutumie nafasi hii ya leo vizuri ili kuweza kupiga hatua kwenye maisha yetu.
Msingi wetu wa maisha ya mafanikio ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA ambapo tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari MARA YA MWISHO KUFANYA…
Kuna mtu anapumua kwa mara ya mwisho sasa, lakini hajui hilo.
Kuna mtu anawasiliana na wale wa muhimu kwake kwa mara ya mwisho, lakini anafikiria atapata nafasi nyingine ya kufanya hivyo.
Kuna mtu anapata nafasi ya kufanya kitu lakini anaahirisha, akijua kesho pia ipo, kumbe leo ni mara ya mwisho kwake kupata nafasi hiyo.
Rafiki, kila mmoja wetu kuna mara ya mwisho ya kufanya vile ambavyo tunafanya, lakini mara nyingi huwa hayujui mara ya mwisho ni wakati gani.
Hivyo tumekuwa tunafanya vitu juu juu tukiamini kuna nafasi nyingine tena ya kufanya.
Lakini kama tutaambiwa hiyo ndiyo mara ya mwisho, tutafanya kwa utofauti, tutaweka kilantulichonacho na tutahakikisha tumeacha alama fulani.
Sasa kwa kuwa mara ya mwisho ipo, lakini hayuijui, kwa nini tusifanye kila tunachokifanya kama ndiyo mara ya mwisho kufanya?
Hii itatusaidia kufanya kitu kwa utofauti mkubwa, kuweka juhudi kubwa na kuacha alama ya kipekee.
Ukijua kwa hakika nafasi uliyoipata ni ya mwisho, hutaipoteza au kuifanyia kazi vibaya. Utaitumia vizuri ili uweze kupata matokeo bora sana.
Chochote unachofanya kwenye maisha yalo, chukulia kwamba ni mara ya mwishi na nafasi ya mwisho kwako kufanya, hivyo kifanye kwa utofauti na upekee wa hali ya juu.
Uwe na siku bora sana ya leo.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha