Ukweli ni kwamba, moja ya njia rahisi za kukubali kushindwa, ni kufanya kile ambacho kila mtu anafanya, kwa namna ambavyo kila mtu anafanya. Hili halikutofautishi kwa namna yoyote ile, badala yake linakuletea msongo, kwa sababu unakuwa katikati ya kelele za wengi.
Hivyo ni muhimu kuwa tofauti kama unataka kujitengenezea kitu chako hapa duniani na hata kufanikiwa.
Lakini kwenye kuwa tofauti pia lazima uwe makini, kwa sababu siyo kila utofauti utakaofikiria utakuwa bora kwako.

Watu wengi wamekuwa wakikimbilia kufanya vitu tofauti kwa sababu tu wanataka kuonekana wako tofauti, hata kama hicho wanachofanya tofauti hakina manufaa kwao.
Kwa sababu kila mtu anatembea kwa miguu, haimaanishi inabidi utembee kwa mikono ili kuwa tofauti. Badala yake unaendelea kutembea kwa miguu, lakini unaweza kutembea kwa mwendo wa kasi kuliko wengine, ukatembea kwa uchangamfu na kujiamini kuliko wengine na kadhalika.
SOMA; UKURASA WA 1024; Kuna Wewe Mmoja Tu Hapa Duniani, Mtumie Vizuri…
Kadhalika kwenye yale tunayoyafanya, tuangalie utafauti unaotufanya kuwa bora zaidi, utofauti unaotusogeza karibu zaidi na malengo na mipango tuliyonayo kwenye maisha yetu. Hili ndiyo muhimu zaidi.
Kuwa tofauti kuwa bora, kuwa tofauti kuongeza thamani zaidi kwa wengine, na usiwe tofauti kwa sababu unataka uonekane ni wa tofauti. Mambo mengi ambayo watu wanafanya ili kuonekana, huishia kuwaumiza badala ya kuwasaidia.
Wakati mwingine kuwa tofauti kunakutaka uvunje baadhi ya sheria na taratibu ambazo watu wamezoea. Hapo pia yakupasa uwe makini, kwanza ujue kwa hakika sheria na taratibu hizo, na unapovunja, uwe na mbadala ambao ni bora zaidi. Usitake tu kuvunja kwa sababu hukubaliani na utaratibu huo, kuwa na kitu bora zaidi.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog