Changamoto kubwa ya zama hizi ni kwamba karibu kila kazi ina watu wengi wanaoweza kuifanya kuliko wanaohitajika, hivyo malipo yanakuwa madogo kwa sababu ukikataa kufanya, wapo wengi ambao wapo tayari kufanya kwa malipo kidogo.

Kwenye biashara pia, hali ni hiyo hiyo, karibu kila biashara inafanywa na kila mtu, na watu wapo tayari kupunguza bei ili kuvutia wateja wengi zaidi. Mwisho mnajikuta mpo kwenye biashara inayowachosha lakini fedha hamzioni.

Kadiri siku zinavyokwenda ndivyo hali hii inavyoshamiri, ndivyo wenye utaalamu wa kila aina ya kazi wanakuwa wengi na ndivyo watu wengi zaidi wanaingia kwenye kila aina ya biashara. Ni rahisi kuona kwamba hakuna tena kazi au biashara inayoweza kulipa.

Tatizo kubwa

Lakini zipo. Zipo kazi na biashara ambazo zitaendelea kulipa zaidi na zaidi. Kazi na biashara hizi ni zile zinazohusisha kutatua changamoto ngumu na kubwa, kutatua matatizo makubwa yanayowasumbua watu, ambayo hakuna mtu anajisumbua nayo.

Kazi na biashara hizi ni zile zinazohusisha kufanya mambo makubwa, magumu na hatari, ambayo kwa kuyafanya mtu unaweza kushindwa. Kazi hizi zinahusisha kufanya vitu ambavyo hakuna mwongozo wa jinsi ya kuvifanya, na hata huwezi kutafuta kwenye google ukapata mwongozo.

Hizi ndiyo kazi na biashara ambazo zitaendelea kulipa zaidi na zaidi. Kwa sababu ni wachache sana ambao wapo tayari kufanya yale ambayo hayana mwongozo, yale ambayo kuna uwezekano mkubwa wa kushindwa na yale ambayo hata ukitafuta google, hakuna suluhisho unalopata.

SOMA; BIASHARA LEO; Biashara Inaanza Kushindwa Ndani Na Siyo Nje…

Utajiuliza unajuaje au kupata wapi kazi na biashara za aina hii?

Na majibu yapo wazi, angalia watu wanaokuzunguka, angalia mazingira unayoishi na iangalie dunia kwa ujumla, utaona matatizo na changamoto nyingi ambazo watu amekubali kuishi nazo na kuona ni sehemu ya maisha. Wewe ukikataa kuzikubali na kuanza kuzitatua, utajiweka kwenye nafasi ya ushindi.

Lakini kumbuka pia nafasi za kushindwa ni kubwa na nyingi, hivyo usikate tamaa, kadiri utakavyoweka juhudi na kuendelea, ndivyo unavyotengeneza nafasi kubwa ya kushinda.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog