Inapokuja kwenye mafanikio yako, kuna wakati inakuwa vigumu kumwamini mtu yeyote kutokana na tabia ya kigeugeu ambayo watu wengi wanayo.

Kwa hakika watu wanapenda kuhusishwa na vitu vinavyofanikiwa, na hawapendi kuwa sehemu ya vitu vinavyoshindwa.

Mtu mmoja aliwahi kusema kwamba mafanikio yana wazazi wengi, ila kushindwa ni yatima. Ukifanikiwa kila mtu atapenda kuwa na wewe, kila mtu atasema alikuwa na mchango kwenye mafanikio yako. Lakini ukishindwa kila mtu atakukimbia, kila mtu atajitenga na wewe.

wp-image--1475273682

Unapoanza safari ya mafanikio, watu wanakuwa na wasiwasi na wewe, licha ya kuwa na mipango mizuri na mikubwa, watu ndani wanajua ni vigumu sana kufikia mipango hiyo.

Lakini hawataki kukukatisha tamaa, hivyo wanakupa moyo, huku ndani wakijua unashindwa. Sasa wanaanza kukupa ushauri ambao wewe unaweza kuona haukufai kulingana na kile unachofanyia kazi wewe. Halafu watataka ufuate ushauri kama wanavyokupa.

Usipofuata ushauri wao, wanakuwa wanaombea ushindwe ili ujue umuhimu wa ushauri wao.

Inapotokea umefanikiwa, wanakuwa wa kwanza kusema wamechangia sana mafanikio yako. Pengine wanasema bila wao usingefanikiwa.

Ikitokea umeshindwa, watakuwa wa kwanza kusema umeshindwa kwa sababu hujafuata ushauri wao kama walivyokupa. Kwamba ungefuata walichokuambia basi ungefanikiwa na kupiga hatua kubwa.

SOMA; UKURASA WA 519; Barabara Lazima Zifagiliwe…

Hichi ndiyo kigeugeu ambacho watu wanacho kwenye mafanikio yako. Kikubwa cha kujifunza hapa ni iwe utafanikiwa au utashindwa, kwa sehemu kubwa upo peke yako. Wengi wanaokuambia tupo pamoja, hutawaona wakati umeshindwa.

Nakukumbusha hili rafiki ili usishangazwe pale uliokuwa unawategemea wawe upande wako wanapokuacha. Pia jua hili ili uwe makini na kila ushauri unaopokea, hakuna ushauri mmoja ambao ukiufanyia kazi basi kila kitu kitakwenda vizuri. Changamoto ni nyingi na kila kitu hakitakwenda kama ulivyopanga au unavyotaka.

Pambana na usikatishwe tamaa na wale wanaosema hujafanikiwa kwa sababu hujafuata ushauri wao, jifunze na piga hatua zaidi. Watu hawataacha kusema yale wanayojisikia kusema.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog