Kama ipo njia ya uhakika ya kushindwa na kupoteza kwenye maamuzi yoyote ambayo mtu anafanya, ni kuendeshwa na tamaa. Yaani tamaa ikishawaka, basi lazima mtu apoteze, ni lazima.

Anaweza asipoteze kwa wakati huo, akapata kile alichotamani, lakini hilo likamkosesha vitu vingi na vizuri vya baadaye.

wp-image--1288404680

Tamaa inapokuwa juu, mtu anashindwa kufanya maamuzi sahihi, kwa sababu anakuwa hafikiri sahihi. Tamaa inaleta upofu wa kifikra, mtu anashindwa kuona zaidi ya ile tamaa ambayo anayo. Mtu anasukumwa kuitimiza tamaa aliyonayo kwa wakati huo, bila ya kujali madhara ya mbeleni kwa kile atakachopata.

Ni muhimu sana kudhibiti tamaa yako, na muhimu zaidi, ni muhimu kujua wakati gani tamaa imekutawala na kuepuka kufanya maamuzi katika wakati huo. Ni vigumu kujua wakati halisi tamaa imekushinda, na ni vigumu zaidi kufanya maamuzi ya kuacha wakati tamaa imeshawaka. Lakini unapaswa kujijengea uwezo wa kufanya hivyo.

SOMA; UKURASA WA 862; Wanachosema Na Wanachofanya….

Umewahi kusikia mtu anasema amefanya kitu lakini siyo kwa akili zake, wengine watasema shetani aliwatuma na sababu nyingine kama hizo. Ukweli ni kwamba, tamaa ikishatawala, na tamaa ikishakuwa kali mtu anaweza kufanya maamuzi ambayo baadaye atasema hajui aliyafanyaje. Kadiri tamaa inavyokuwa kali, ndivyo akili inavyoshindwa kufanya kazi.

Muhimu zaidi yajue mazingira yanayoamsha tamaa zako, kisha jikinge nayo, au jipe masharti na sheria za kufuata katika mazingira hayo. Hilo litakusaidia kuanguka pale tamaa zinapowaka ndani yako.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog